Rufaa hiyo imekatwa na aliyekuwa mfanyakazi wa mbunge huyo, Hashim Ally anayemtuhumu mwajiri wake huyo wa zamani kumfanyia ukatili akimtuhumu kuwaelekeza vijana wake kumvua nguo na kumwingizia chupa ya soda katika njia ya haja kubwa.
Akizungumza na Mwananchi, Jumamosi Januari 27, 2024, wakili wa Hashim, Peter Madeleka amethibitishia kuhusu wito huo.
Gekul ambaye kabla ya kuibuka kwa tuhuma hizo dhidi yake alikuwa Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumamosi Januari 27, 2024 alipozungumza na Mwananchi Digital kwa simu kuhusu hilo, amesema hajaipata hati hiyo.
Pia, amehoji inakuwaje nyaraka za Mahakama zinawahi kupatikana kwenye mitandao wakati mhusika hajaipata.
“Mimi sijapata brother (kaka). Najua mambo ya Mahakama yana taratibu zake, inakuwaje nyaraka za Mahakama zinawahi kwenye mitandao kabla mhusika hajaipata? Kwa hiyo sifahamu chochote,” amesema Gekul.
Katika rufaa hiyo ya jinai namba 577, Hashim anapinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Babati kuifuta kesi yake aliyokuwa amemfungulia mbunge huyo, kufuatia taarifa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kutokuwa na nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya wito wa Mahakama hiyo kwa Gekul iliyosainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Januari 18, mwaka huu, ambayo Mwananchi imeiona nakala yake jana, rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa na Jaji Stephen Magoiga.
“Fahamu kwamba siku ya Machi 18, 2024, saa 3:00 asubuhi imepangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa rufaa iliyokatwa na mrufani katika kesi iliyotajwa hapo juu (Hashim Ally), mbele ya Jaji S.M Magoiga,” inasomeka hati hiyo kwa tafsiri isiyo rasmi.
Hatua hiyo ya kupangwa kusikilizwa kwa rufaa hiyo imekuja huku DPP Sylvester Mwakitalu, akiwa ameshaweka msimamo wake kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kimakosa hivyo, yeye ndiye mwenye dhamana na hajashindwa kufungua upya kesi hiyo.