Jeshi la Polisi mkoa Arusha linamshikilia Mkaguzi msaidizi wa Polisi kituo cha USA River, Demetrida Thadeo kwa tuhuma za kukodi watu wanaodhaniwa ni majambazi ili kumuua mumewe, Daudi Ayo kutokana na ugomvi wa wanandoa hao.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa watu hao hawakufanikiwa kumuua, baada ya majirani kuwahi kumwokoa na kumkimbiza hospitali.
Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo kuzungumzia suala hilo hazikufanikiwa, lakini chanzo ndani ya jeshi hilo mkoani hapo kilieleza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na ukikamilika taarifa rasmi itatolewa.
"Kamanda atatoa taarifa uchunguzi ukikamilika mpaka sasa hatuna taarifa yoyote," kimesema chanzo hicho.
Alipoulizwa na Mwananchi leo Januari 6, 2024, Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime amesema taarifa hizo walizipata na wanakusanya taarifa.
“Jeshi la Polisi lilipokea tuhuma dhidi ya askari huyo na hatua zilianza kuchukuliwa siku hiyo hiyo ikiwa ni pamoja na kumhoji na kukusanya ushahidi wa watu wengine na wa kielektroniki ili kupata ukweli.
“Endapo itabainika ni kweli na kwa sababu hakuna aliye juu ya sheria kutokana na vitendo binafsi, hatua zingine za kimahakama zitafuata,”amesema.
Akizungumza na waandishi wa habari leo baba mzazi wa Daudi, Thomas Ayo amesema mtoto wake amejeruhiwa vibaya kwa mapanga na vijana wanaodaiwa kutumwa kumuua.
Amesema watu hao wanne walimvamia kijana wake wakati anataka kuingia nyumbani getini na kuanza kumkata mapanga kichwani na mikononi na alipoanguka chini walijua tayari amekufa.
"Bahati nzuri watu walijitokeza na kumuokoa kumpeleka hospitali na baadaye mkewe wake alinipigia simu kuwa kijana wangu ameshambuliwa na wezi," amesema.
Amedai jaribio hilo la mtoto wake kuuliwa ni la tatu kukwama, kwani tayari yaliwahi kufanyika majaribio mawili na kushindwa.
Amedai kwa muda mrefu askari huyo na kijana wake wamekuwa na ugomvi wa kifamilia ambao kwa kiasi unatokana na wivu wa mapenzi.
Hata hivyo, majeruhi huyo ambaye hufanya kazi katika kampuni ya udalali wa mashamba ya Kambele, hakupatikana kueleza kilichompata, baada ya ndugu kueleza kuwa amelazwa hospitali ya ALMC (Selian), jijini humo akiwa na hali mbaya.