Achana na Profesa Janabi, Big Boss wa Muhimbili pale. Ambaye kwa sasa amekamata namba 'wani oni trendingi' kitaa cha insta na 'eksi'. Kutokana na maonyo yake yaliyokosa soko kwenye masikio ya wengi. Kifupi mwamba huyu anaturusha sana stimu zetu.
Watu wanawaza biere, nyama choma na pisi kali. 'Faza' huyu aliyehifadhi kichwani mwake elimu kubwa ya udaktari wa binadamu. Anatuletea stori za kisomi zenye kichomi kuhusu nini cha kula na nini cha kuacha. Ajabu elimu yake inaelekeza tule misosi ya mbuzi.
'Okei' siyo kesi. Sasa ndio kipindi hiki ambacho akili na mawazo yetu yapo kwenye kuchoma pesa kwa pombe na nyama choma? Yaani sikukuu hizi uniletee ngonjera na pambio za kunde, kabechi na maji ya kutosha? Hebu kuwa 'siriazi' Janabi.
Tunakoelekea atatuambia kuzipenda Simba na Yanga unapoteza nguvu za kiume. Na ndio utakuwa mwisho wa mabandiko ya vitisho vyake. Maana raia zitakosa uaminifu. Aendelee kutuonya kwa mitungi na misosi, ambayo wana kitaa wanafakamia kupitiliza.
Sasa leo namuongelea Profesa Jay na siyo Janabi. Aliyekuwa mbunge wa watu na wanyama Mikumi. Aliyelala kitandani kwa zaidi ya mwaka akipagania afya yake. 'Lijendi' wa Bongofleva. Yes! ‘Machozi Jasho na Damu’ na mwana mapinduzi halisi wa muziki huu.
Kuanzia 2000 baada ya pini la 'Chemsha Bongo'. Kutoka ndani ya albamu ya 'Funga Kazi', chini ya 'Kikosi Kazi' cha Hard Blasters (HBC). Profesa Jay aliendelea kulifanya 'gemu' lisonge kwa kumzunguka yeye. Alikuwa kama Mayele na Yanga ya msimu uliopita.
Pini juu ya pini na zote za moto. Kuna wakati alikamata nafasi za juu kwenye chati kibao za muziki redioni. Tena kwa nyimbo zake nyingi kuingia kwenye 'topu teni ama topu twenti kama siyo topu fifte' na kuendelea. Utaweka 'Jina Langu' halafu 'Piga Makofi' unamuachia nani?
Utaweka 'Bongo Dar es Salaam' na 'Ndiyo Mzee' uende wapi? Ndivyo ilivyokuwa kwa pini kama 'Nawakilisha' 'Niamini', 'Piga makofi' na nyingine. Jay alifanya wasanii wengi walisusie 'gemu' na wasanii wengi waingie kwenye 'gemu' kwa sababu yake. Huu ndiyo ukweli.
Waliosusa na kuendelea na mishe zingine. Ni wale ambao walihofia uwezo wake mkubwa wa kuandika. Walihisi kwamba hawawezi kufanya kama yeye. Kabla hujaingia studio kama ngekutana kitaa na watu wanapiga ngoma zake ingekutisha sana.
Kama una akili timamu lazima ujiulize kwamba nitaweza kuwashika watu kama jamaa alivyowashika? Na kawashika kwa sababu gani? Ukigundua kuwa ni kwa sababu ya uwezo wake wa kuandika ngoma kali. Hapo ungekosa nguvu ya kuendelea na 'gemu'.
Lakini wakati huohuo wasanii kibao walipata mzuka wa kufanya muziki baada ya balaa la Profesa Jay. Kwanza aliwafanya wazazi wengi waamini muziki huu siyo wa kihuni. Na zaidi ni muziki unaoelimisha na kuburudisha jamii. Nyakati zimeenda kwa kasi sana.
Kuna wakati unasikiliza ngoma za sasa unashangaa. Unajiuliza hizi 'singo' zingetoboa vipi mbele ya 'Promota Anabipu'? Ni vipi 'wangebato' na pini kama ‘Bongo Dar es Salaam’? Kuna kuandika na kuandika kulikopitiliza. Na zaidi staili za michano.
Na msingi alioujenga, ndio unaomlinda sasa. Alipoitwa 'Dadi' na kina Ngwea walimaanisha. Alipoitwa 'The Heavy Weight Mc' na kina Mwana FA, 'hawakufeki' walimaanisha na huo ndio ukweli. Uzito wa Jay ni wa juu sana kulinganisha na wenzake.
Ndiyo maana leo anatoka kitandani alikolala zaidi ya mwaka. Anakuja kitaa, anaanzisha jambo na raia wanafuata. Kwa sababu ya msingi wa nyuma alioujenga kwenye nyoyo za raia. Alifundisha, aliponya na kuwezesha wengi kupitia tungo zake.
Leo hii anabaki kuwa mwanamuzki ambaye kafunga mwaka kibabe. Kila kitu alichoshika au kukishiriki mapokeo yamekuwa makubwa sana. Ni kama vile tulikuwa naye kitaa siku zote, kumbe mwamba alikuwa kalala muda mrefu na mtaa umempokea.
Huyu ndiye 'Mani ofu ze mechi' kwenye gemu mwaka huu. Haya mambo hayaji kwa bahati mbaya. Watu walivuja jasho jingi na damu nyingi kwenye ujenzi wa jumba linaloitwa Bongofleva. Sema Jiiiiiiiiiiiiaaa....