Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametengua nafasi ya Kamishna wa Petroli na Gesi chini ya Wizara ya Nishati, Michael Mjinja bila kuweka wazi sababu za utenguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Januari 4, 2024 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus imesema; “Mjinja atapangiwa kazi nyingine.”
Mjinja amehudumu katika nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili.
Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015, majukumu ya kamishna ni kumshauri waziri mwenye dhamana ya petroli kuhusu masuala ya kisera, mipango, miongozo pamoja na majukumu ya kiutendaji ya kila siku kwenye sekta ndogo ya gesi na mafuta.
Miongoni mwa majukumu hayo ya kiushauri ni pamoja na eneo la matumizi ya nishati safi ya kupikia, uendelezaji wa miradi mikubwa ya gesi asilimia na uwezeshaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Eneo lingine ni ushauri kuhusu uchumi unaotokana na utajiri wa gesi asilia, udhibiti na uratibu wa biashara na huduma za mafuta nchini, pamoja na suluhisho la changamoto za nishati ya umeme.
Rais Samia anafanya mabadiliko hayo katika sekta hiyo ya nishati ikiwa ni mwendelezo wa mabadiliko kadhaa anayofanya kwa nafasi za watendaji wa taasisi.
Miongoni mwa mabadiliko ni pamoja na viongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).