WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) umewataka wananchi wapuuze taarifa zilizozagaa katika baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii zinazowataka wanandoa wote kwenda ofisi zao kusajili ndoa zao. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
RITA imesema wanandoa wenye vyeti vya ndoa vya serikali ndoa zao zimesajiliwa na hawana sababu ya kwenda ofisi kusajili tena ndoa zao.
Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi
Akizungumza na waandishi wa habari hapa, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi, ameeleza kuwa wanandoa wenye vyeti vya ndoa vya serikali ndoa zao zinatambuliwa na sheria.
“Napenda ieleweke kwamba wanandoa ambao wamefunga ndoa za kidini, kiserikali au kimila na kupewa vyeti vya ndoa vya serikali, ndoa zao zimesajiliwa kwa mujibu wa sheria,”alisisitiza.
Kanyusi alirejea Sheria ya Ndoa, Sura ya 29 kifungu cha 30, 43 na 46 na kueleza kuwa RITA ina taarifa zote za ndoa ambazo wanandoa wamepewa vyeti vya ndoa vya serikali na kwa hiyo wao kama Msajili Mkuu wanaweza kutoa nakala nyingine endapo wanandoa watapoteza vyeti walivyopewa awali na wafungishaji ndoa.
Amesema wanawataka wafungishaji ndoa kuhakikisha wamesajili kwenye mfumo wa RITA wa kieletroniki kupitia eRITA kwani wanaweza kupata huduma hiyo popote walipo nchini.
Aidha wahakikishe wanahuisha leseni zao za kufungisha ndoa kwa wakati na wahakikishe wanasajili ndoa zote pindi zinapofungwa na kuwapa wanandoa vyeti na wahakikishe wanafanya marejesho ya ndoa walizofunga kila mwezi ili Msajili Mkuu aweze kuwa na taarifa au rekodi ya ndoa zote zinazofungwa kwa wakati.
Amesema RITA imeweka mkazo kwenye kuwasajili watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano nchi nzima chini ya mpango maalumu wa kuwasajili wa watoto katika ofisi za kata na kliniki za mama na mtoto.
Kanyusi alieleza kuwa kumekuwapo changamoto ya kukubaliwa vyeti katika baadhi ya taasisi za umma na binafsi na wananchi kupata usumbufu.
“Napenda ieleweke kwamba vyeti vilivyojazwa na mkono vina uhalali sawa na vyeti vingine vinavyotolewa na kompyuta hivyo vinafaa kwa matumizi yote… RITA ndiye mwenye dhamana na mamlaka ya kutoa vyeti vya kuzaliwa ikiwa ni pamoja na kuvihakiki.
Iwapo kuna mashaka yoyote juu ya vyeti vyote vinavyotolewa na ofisi yetu nawaomba muwasiliane nasi kwa ajili ya ufafanuzi, uhakiki pamoja na kuthibitisha uhalali wa nyaraka hizo,” amesema Kanyusi.
Amezitaka ofisi za serikali na binafsi kuvipokea vyeti na kuwapatia wananchi hudumu bila usumbufu wowote.