Bingwa wa Mapinduzi Hakuwahi Kutetea Wala Kubeba Ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba Leo Kujiwekea Kimavi

 

Simba Kuachana na Ubingwa wa Ligi Kuu Bara leo

Rekodi haziongopi na leo zinakumbusha kitu kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi itakayochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini hapa kati ya Simba na wenyeji, Mlandege kuanzia saa 2:15 usiku.


Ni hivi kwa mujibu wa rekodi za miaka kumi iliyopita, bingwa wa Mapinduzi hakuwahi kutetea wala kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara. Yanga ilijaribu mara moja tu mwaka 2007 ikabeba kotekote na gundu likaanza tangu mwaka 2008.


Rekodi hizo zimeibua maswali kwa baadhi ya wadau haswa wa Simba ambao wamepania kubeba ubingwa mbele ya Mlandege huku dhamira kubwa ikiwa ni taji la Ligi Kuu Bara. Swali ni je, wakibeba leo Mapinduzi rekodi zitawaandama au watazifuta kama Yanga ilivyofanya 2007? Angalia takwimu zilizopo katikati ya ukurasa huu.


Balaa hilo la kupoteza ubingwa wa Ligi ya Kuu timu inapotwaa Kombe la Mapinduzi haipo kwa timu za Tanzania Bara pekee. Mwaka 2009 ambao Miembeni ilitwaa ubingwa wa Mapinduzi, haikubeba ule wa Ligi Kuu Zanzibar kwani taji hilo lilikwenda kwa Mafunzo na mwaka jana ambapo Mlandege ilibeba ubingwa wa Mapinduzi, taji la Ligi Kuu lilikwenda kwa KMKM. Na hizo ndizo mara mbili pekee ambazo timu za Zanzibar zilitwaa ubingwa wa Mapinduzi.


MECHI YENYEWE


Leo ni bonge la mechi pengine kuliko fainali iliyopita ya Mapinduzi 2023 iliyoikutanisha Mlandege dhidi ya Singida Big Stars (sasa Fountain Gate) ambayo mwaka huu imetolewa hatua ya nusu fainali na Mnyama.


Ni kati ya bingwa mtetezi dhidi ya Simba katika fainali inayosubiriwa kwa hamu zaidi ya Krismasi au Idd El Fitr.


Baada ya michezo 24 kuanzia makundi mpaka nusu fainali timu hizo mbili zicheza mchezo wa 25 wa fainali hiyo inayotabiriwa kuwa ngumu kwa timu zote.


Mlandege ambayo ni kama mwenyeji ni timu inayoonekana kuwa na mashabiki wengi mjini hapa ikitokea kundi A, ikirudi kwenye fainali na dhamira mbili. Kwanza kutetea ubingwa iliouchukua msimu uliopita mbele ya Singida Fountain Gate ambayo Simba ndio iliyowatumia kutinga fainali.


Akili ya pili ya Mlandege ni kuendeleza ubabe mbele ya Wekundu hao kwenye mchezo huo utakaoanza saa 2:15 usiku.


Changamoto kubwa ya Mlandege ni eneo la ushambuliaji ambapo hakuna mchezo msimu huu wa mashindano hayo imeshinda au kuweka kambani mabao mawili ndani ya dakika 90 ikitoka sare mechi zote kuanzia makundi mpaka fainali ikifuzu hatua zote za mtoano kwa matuta.


Timu hiyo iko vizuri kwenye eneo la ukuta ambao pia haujaruhusu bao zaidi ya moja kwenye mechi zote za msimu huu wala kupoteza mchezo.


Mlandege inaringia rekodi yake mbele ya Simba ambapo timu hizo zinakutana mara ya nne kwenye historia ya mashindano hayo ambapo imeshinda mechi moja na mbili kutoka sare - rekodi ambayo Simba italazimika kuanzia hapo kuhakikisha inabadilisha mambo.


MNYAMA KAPANIA


Simba inalitaka kombe hilo na wala haitaki kuficha matokeo ya uwanjani na jinsi inavyopambana ni jibu tosha kwamba Mlandege inakwenda kucheza mechi ngumu dhidi ya Wekundu.


Simba ilitinga fainali ikiwa na mabao saba ya kufunga na kuruhusu mawili, ikitoka sare mechi mbili ilhali zingine tatu ikishinda ikiwa na safu nzuri inayofunga, lakini pia ukuta imara.


Timu hiyo inautaka ubingwa wa tano wa mashindano hayo msimu huu na mchezo wa nusu fainali dhidi ya Singida Fountaina Gate ilionyesha kiu hiyo kwa vitendo kwani ilisawazisha bao jioni na kwenda kukata tiketi ya fainali kwa matuta.


Simba inaweza kuwa na badiliko moja kwenye kikosi cha leo akiingia beki Hussein Kazi kuchukua nafasi ya Kennedy Juma ambaye kocha Abdelhak Benchikha anaamini bado anahitaji utulivu kidogo kufuatia makosa aliyofanya kwenye mchezo dhidi ya Singida.


Husein alicheza dakika 45 za mechi dhidi ya Singida na hapana shaka alionyesha kwamba anaweza kumudu majukumu ya mchezo wa leo dhidi ya Mlandege.


Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola akizungumzia mchezo huo alisema wanatarajia kucheza fainali ngumu dhidi ya Mlandege ambayo inahitaji heshima kwani imefika fainali.


“Ni kweli rekodi zinatuhukumu mbele ya Mlandege, lakini tumejipanga kucheza fainali ngumu dhidi yao. Kila timu inayofikia hapa inahitaji heshima. Tunajivunia kikosi chetu na maandalizi ya siku mbili hizi ambazo angalau zimewatoa uchovu wachezaji,” alisema Matola.


“Tunahitaji kwenda kushinda kila kinachotakiwa kufanywa na sisi makocha tumekifanya, na sasa imebaki nafasi ya wachezaji kwenda kukamilisha kazi mbele ya mashabiki wetu.”


Nahodha wa Mlandege, Sabri Ramadhan Mzee maarufu kwa jina la China alisema wachezaji wa ari kubwa kwani fainali ni fainali na chochote kinawezekana kutokea.


“Hakuna timu nyepesi. Kama tulipambana kutoka mwanzo hadi kufikia hapa, basi tutakwenda kupambana pia katika mchezo huo,” alisema China.


Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, kipa wa Simba, Ally Salim alisema wamejipanga vizuri na wapo tayari kwa lolote.


Ikumbukwe msimu uliopita wa Kombe la Mapinduzi timu hizo zilikuwa kundi moja - kundi C na zilipokutana Januari 3, 2023 Mlandege ilifanikiwa kutoka na ushindi wa baop 1-0 ambalo lilitupiwa kimiani na Abubakar Mwadini katika dakika ya 75.


MWINYI NDANI


Michuano hiyo itafungwa rasmi leo hii na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi ambaye atakuwa mgeni rasmi na bingwa anatarajiwa kuondoka na Sh100 milioni, huku mshindi wa pili akipata Sh70 milioni.


Katika Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia jana baada ya shamrashamra za sherehe za Mapinduzi kumalizika kulikuwa na ulinzi mkali.


Hii itakuwa fainali ya kwanza ya Mapinduzi kupigwa katika uwanja huo ambao umefanyiwa maboresho makubwa na kuufanya uwe wa kisasa zaidi na hivyo timu hizo mbili zinatarajiwa kuandika historia kuwa za kwanza kuutumia kwa ajili ya mchezo wa fainali.


FAINALI ZILIZOPITA 2007... Yanga 2-1 Mtibwa Sugar 2008... Simba 1-0 Mtibwa Sugar 2009... Miembeni 2-0 KMKM 2010... Mtibwa Sugar 1-0 Ocean View 2011... Simba 2-1 Yanga 2012... Azam 3-1 Jamhuri 2013... Azam 2-1 Tusker FC 2014... KCCA 1-0 Simba 2015... Simba 0-0(4-3) Mtibwa Sugar 2016... URA 3-1 Mtibwa Sugar 2017... Azam 1-0 Simba 2018... Azam 0-0 (4-3) URA 2019... Azam 2-1 Simba 2020... Mtibwa Sugar 1-0 Simba 2021... Yanga 0-0 (4-3) Simba 2022... Simba 1-0 Azam 2023... Mlandege 2-1 Singida BS 2024... Mlandege ??? Simba

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad