Shirikisho la Soka nchini Tanzania (TFF) limemsimamisha kazi kocha wa timu ya taifa ya wanaume Taifa Stars, Adel Amrouche.
Raia huyo wa Algeria ameonyeshwa mlango kutokana na matamshi yake dhidi ya timu ya Morocco baada ya kudai kuwa timu hiyo maarufu kama Atlas Lions ina ushawishi ndani ya Shirikisho la Soka la Africa (CAF) na hivyo basi imekuwa ikishirikiana na waamuzi kupanga matokeo ya mechi.
Amrouche, ambaye kwa wakati mmoja aliinoa timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, alitoa matamshi hayo masaa machache kabla ya timu yake kumenyana na Morocco katika mechi yao ya ufunguzi ya kuwania ubingwa wa dimba la AFCON linaloendelea huko Ivory Coast.
Vijana hao wa Rais Samia Suluhu Hassan walipojimwaya uwanjani, mnamo Januari 17, 2024, walirindimwa magoli matatu kwa nunge.
Kufuatia matamshi dhidi ya kikosi cha Morocco, Shirikisho la Soka la Morocco (RMFF) liliandikia CAF kumripoti Amrouche kuhusu kauli yake.
Kamati ya Nidhamu ya CAF ilimpiga faini kocha huyo asiongoze kikosi chake katika mechi nane.
“RMFF ilimlalamikia kocha huyo kwa kauli zake kuwa Morocco ina ushawishi ndani ya CAF katika kupanga mechi pamoja na waamuzi. Katika hatua nyingine, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemsimamisha kocha Adel Amrouche,” ilisema sehemu ya tarifa iliyotiwa saini na afisa wa habari na mawasiliano wa TFF Cliford Mario Ndimbo.
Kufuatia uamuzi huo, shirikisho hilo lilimkabidhi Hemed Morocco mikoba ya kuiongoza Taifa Stars kwa michuano yake iliyosalia katika kinyang’anyiro hicho japo kwa ukaimu. Hemed atasaidiwa na Juma Mgunda.
Kwenye mechi zake mbili za kundi zilizosalia, wawakilishi hao wa pekee wa Afrika Mashariki katika kombe hilo watavaana na Zambia Jumapili (Januari 21, 2024) kabla ya kumaliza udhia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumatano (Januari 24, 2024)
Taifa Stars wanavuta mkia katika kundi F bila alama yoyote baada ya kusakata mtanange mmoja. Morocco wanaongoza kundi hilo kwa alama tatu. Timu za DRC na Zambia zina alama moja kila mmoja katika nafasi ya pili na tatu mtawalia.