Try Again: Tunaendelea Kushusha Wachezaji Wapya Simba




Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ ameahidi kushusha wachezaji wengine wapya wenye ubora kuhakikisha kikosi chao kinakuwa tishio katika msimu huu 2023/24.

Simba SC hadi hivi sasa tayari imekamilisha usajili wa wachezaji watatu ambao ni viungo Babacar Sarr, Ladack Chasambi na Salehe Karabaka ambao tayari wametambulishwa na timu hiyo.

Hiyo ni katika kuhakikisha wanafanya vema katika msimu huu ikiwemo kubeba Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufika hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Salim amesema kuwa bado hawajakamilisha usajili katika dirisha dogo, licha ya kusajili wachezaji watatu hadi hivi sasa ambao wote pendekezo la Kocha Mkuu Mualgeria, Abdelhak Benchikha.

Salim amesema kuwa wamepanga kuendelea kushusha wachezaji wengine wapya, watakaokuja kukiimarisha kikosi chao katika michuano yote wanayoshiriki katika msimu huu ambao wamepanga kubeba mataji yote watakayoshiriki kwa kuanzia Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ameongeza kwa kuupongeza usajili wa kiungo mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Chasambi baada ya kuchukua maamuzi sahihi ya kuichagua Simba SC, kukata ofa kadhaa alizopelekewa kutoka timu nyingine.

“Tutazidi kukiimarisha kikosi chetu katika dirisha hili dogo, kwa kuendelea kuboresha baadhi ya maeneo ambayo kocha amependekeza kuyaboresha.


“Hivyo tutaendelea kufanya usajili wa wachezaji wapya watakaokuja kukiboresha kikosi chetu katika dirisha hili dogo la usajili, baada ya kupokea ripoti ya usajili ya kocha.

“Niwahakikishie Wanasimba kuwa wachezaji wote tutakaowasajili wote ni tishio, wanakuja kuijenga Simba SC itakayokuwa imara,” amesema Salim.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad