Baada ya Yanga kutoa taarifa za kurejea kwa winga wa zamani wa timu hiyo, Bernard Morrison ‘BM33’, kocha anayemnoa FAR Rabat ya Morocco, Nasredine Nabi amevunja ukimya na kuanika sababu ya kumrejesha Mghana huyo klabuni hapo.
Winga huyo alipewa mkono wa kwaheri na Yanga mwishoni mwa msimu uliopita na kutua FAR Rabat inayonolewa na Nabi kabla ya kuumia na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na juzi kati ameibukia Yanga.
Licha ya kufahamika kama mchezaji mwenye vituko zaidi wakati akiwa na Simba na Yanga, kocha huyo alikiri kuona mabadiliko mazuri ya kinidhamu na kiwango chake kwa jumla katika kikosi hicho cha FAR, ndipo leo tulimpigia simu akiwa Morocco kujua sababu ya BM33 kurudi Yanga.
Kocha huyo aliyeifikisha Yanga fainali za Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, alisema sababu kubwa ya kumruhusu Morrison kurudi Tanzania ni kwa ajili ya matibabu zaidi.
Nabi alisema, amekaa Yanga kwa kipindi kirefu na alikuwa akivutiwa sana na matibabu ya daktari wa viungo wa kikosi hicho, Youssef Ammar, ndio maana akaamua kuruhusu winga huyo kuja kutibiwa hapa kipindi hiki.
“Wakati niko Yanga niliwashuhudia wachezaji kama, Yacouba Songne, Kibwana Shomary na kipa Abutwalib Msheri wakipona kwa haraka, kwani daktari aliyewafanyia upasuaji ndiye huyo huyo aliyemtibu Morrison, hivyo naamini atakuwa sawa,” alisema Nabi na kuongeza;
“Amekuja huku kwa sababu daktari wa viungo wa Yanga, Youssef Ammar, ambaye anajulikana kwa ubora wa kujua kuwasimamia wachezaji wanaotoka kwenye majeraha makubwa na kurudi uwanjani kama awali. Morrison atakuwa hapo nchini chini ya uangalizi wa Youssef kwa kumpa ratiba ya mazoezi hadi atakapokuwa sawa.”
Morrison aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja FAR Rabat, atakuwa nje hadi msimu huu utakapomalizika kama majeraha hayo yatachukua muda zaidi, jambo ambalo linaweza kuweka hatarini kibarua chake ndani ya kikosi hicho kwani bado hakuonyesha makali yake.
Morrison alisajiliwa kwa mara ya kwanza dirisha dogo la msimu wa 2019-2020 kabla ya kukimbilia Simba msimu uliofuata wa 2020-2021 na kuibua mgogoro baina yao kiasi cha kufikishana Fifa na CAS, japo alishinda kesi na kukaa Msimbazi kwa misimu miwili hadi msimu uliopita akarejea Yanga na kucheza nusu na mechi za msimu mzima kutokana na sababu tofauti.
Katika misimu mitatu aliyokuwa Tanzania Morrison amefunga jumla ya mabao 14 katika Ligi Kuu Bara na kutwaa pia mataji manne tofauti yakiwamo mawili ya Ligi Kuu Bara na mengine kama hayo ya ASFC na Ngao ya Jamii mbili pia.