Kusimamishwa kwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Adel Amrouche kumeibua mitazamo tofauti kwa wadau wakiwamo vigogo wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na makocha waliosema hatua hiyo ilipaswa kuchukuliwa mapema na TFF kabla ya CAF kumshughulikia.
Kocha huyo raia wa Algeria, amefungiwa mechi nane na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutokana na kushtakiwa na Shirikisho la Soka la Morocco kwa kauli tata alizotoa juu yao kabla ya TFF nayo kutangaza kumsimamisha, huku ikielezwa kuwa kocha huyo kibarua chake ndio kimeshaota nyasi.
Tanzaniaweb.com jana tuliwajulisha kwamba siku za kocha huyo zinahesabika kabla ya kusitishwa kibarua, lakini maamuzi ya CAF ni kama yameirahisishia kazi TFF kwani tayari wameikabidhi timu kwa makocha wazawa, Hemed Suleiman 'Morocco' na Juma Mgunda kumalizia mechi mbili za Kundi F za Fainali za Afcon 2023.
Kauli zake tata kwa wachezaji, kutoambilika na kuwa na misimamo mikali pamoja na matokeo mabaya kwa Stars ni kati ya vitu vilivyokuwa vinamuondoa Amrouche maperma kabla adhabu alizopewa na CAF na TFF na jambo hilo limewaibua wadau waliotoa mtazamo wao, huku vigogo wa zamani wa TFF wakiunga mkono.
Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Mwesigwa Selestine, amesema kama Stars inaweza ikapata madhara ya moja kwa moja, anaamini kuongezeka kwa Juma Mgunda kwenye benchi la ufundi kutaongeza nguvu kwa Hemed Suleiman 'Morocco' aliyeanza falsafa ya Amrouche watakayoiendeleza kwenye michezo iliopo mbele yao.
Selestine alisema TFF ilichelewa kuchukua maamuzi dhidi ya Amrouche, kutokana na kauli aliyotoa kwa wachezaji baada ya kufungwa mechi ya kirafiki dhidi ya Misiri, ambayo aliiona ni kujitafutia bomu mwenyewe.
"Kuna makocha waongeaji sana, kama Jose Mourinho, lakini huwezi kumsikia akiwatolea kauli ngumu wachezaji kwenye vyombo vya habari, anajua wakifeli ni kufeli kwake, hivyo nilitegemea TFF wangeliangalia hilo tangu kule Misri alichokifanya ni kujitafutia bomu mwenyewe, kocha anaweza akapaniki kama wanafanya vibaya labda mechi tano hivi ila sio moja kama vile," alisema Mwesigwa na kuongeza;
"Siwezi kumhukumu kwa adhabu, kwani ni jambo la kawaida linalowapa wachezaji pia, nakumbuka 2015 aliwahi kupewa adhabu ya kufungiwa mechi mbili akiwa na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars kwa kosa la kumtemea mate mwamuzi."
Katibu mwingine wa zamani wa TFF, Angetile Osiah alisema Amrouche alikuwa anaonyesha kiburi cha wazi mbele ya hadhara na wachezaji wana mambo mengi, inapaswa kuishi nao kwa akili kubwa na sio kuwapuuza.
"Kitu kingine kilichonishangaza ni kumsema hadharani, Kelvin John alipaswa kumuita na kumkanya na sio kuiharibu saikolojia yake, bado ni kijana taifa linamtegemea, ukiachana na huyo maelezo yake juu ya Clement Mzize hayakujitosheleza, huku na kule kauli aliyotoa Misri," alisema Angetile na kuongeza;
"Kocha ukiwa na jeuri kama hivyo na unawategemea wachezaji kufanya nao kazi, sijui alitarajia kitu gani, ingawa kauli dhidi ya Morocco ilikuwa mpango wa mechi ambao ulifeli, kwani nchi hiyo haielewani na Algeria anakotoka.
"Baada ya kusimamishwa natarajia wachezaji watajituma kwa bidii michezo inayofuata, nilimuona nahodha Mbwana Samatta alikosa furaha kutokana na kauli aliyoitoa Misri, wakati huyo ni kiongozi wa wachezaji wenzake angekuwa anasaidiana naye kuwahamasisha, ila kwake haikuwa hivyo."
Ukiachana na viongozi hao, Kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' alisema Morocco na Mgunda anawaamini watafanya kazi nzuri, kikubwa ni kuwajenga wachezaji kiakili wakijua wapo kwa ajili ya kulipambania taifa lao.
"Nyakati kama hizo ziwaongeze ari ya kujituma kwa bidii, Watanzania tupo nyuma yao, tunawaamini wao wanatuwakilisha vizuri, kutokea dharura kama hizo ni jambo la kawaida hata wachezaji wanakutana nazo ndio maana wengine wanapewa kadi nyekundu," alisema Julio, huku kocha mkongwe nchini, Abdallah Kibadeni akisema; "Kocha Morocco bado atakuwa kwenye falsafa za Amrouche, hivyo kuongezeka kwa Mgunda kutaongeza nguvu, kwani wote wanawajua vizuri wachezaji, hivyo watawajenga kiakili kukabiliana na michezo iliopo mbele yao."
Jambo hilo limewagusa wachezaji wa zamani wa Stars kama beki Boniface Pawasa aliyesema "Changamoto kama hizo huwa zinatokea kwenye soka, kwani hata wachezaji wanaweza wakapewa kadi nyekundu, hilo liwape nguvu ya kupambana zaidi na siyo kurudi nyuma."
Mwingine ni Edibily Lunyamila aliyesema "Linapokuja suala la kulipambania taifa, haijalishi ni mazingira gani, licha ya kusimamishwa kwa kocha mkuu, nawaamini makocha waliopo na wachezaji watafanya makubwa."
Habari za ndani kutoka Ivory Coast zinasema asilimia kubwa ya wachezaji wamefurahishwa na kocha mkuu kukaa kando, kwani walikuwa wanavunjwa nguvu, kutokana na kauli zake za dharau alizokuwa anazitoa dhidi yao.