Dodoma. Wakati zikiwa zimesalia siku sita kabla ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufanya maandamano, vyama vya ACT Wazalendo, CUF, NCCR Mageuzi, AAFP, ADC na Demokrasia Makini vimesema havitashiriki na haviungi mkono kufanyika kwake.
Wakizungumza mbele ya waandishi wa habari leo Alhamisi, Januari 19, 2014 Jijini Dodoma, wenyeviti wa vyama hivyo mkoani hapa wamesema kuwa hawaungi mkono maandamano hayo kwani vyama hivyo vina njia zake za kudai haki nje ya maandamano.
Juzi vyama 13, vilijitokeza kupinga maandamano yaliyoitishwa na Chadema, hivyo kujitokeza kwa vyama hivi sita mkoani Dodoma ni mwendelezo wa kutounga mkono kilichosemwa siku chache zilizopita na Mwenyekiti wa Chadema Freeman, Mbowe aliyetangaza mpango huo.
Kati ya vyama hivyo sita vilivyojitokeza jana mkoani Dodoma, ni CUF peke yake yenye diwani mmoja kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Chemba na diwani mmoja Kondoa Vijiji.
Mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Dodoma, Yohana Musa amesema chama chake hakiungi mkono maandamano hayo, kwani chama hicho kina njia zake za kudai haki kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Musa amesema hawatashiriki kwenye maandamano hayo, kwani mpaka sasa bado haijafahamika kama maoni waliyoyatoa kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yamechukuliwa au yameachwa.
“Hayo ni maoni ya Chadema ya kudai haki kwa njia ya maandamano, lakini sisi tunajua Taifa kwanza leo na kesho na kama itatokea maoni yetu hayajachukuliwa tutajua namna ya kufanya na siyo kuiga wenzetu wanachokifanya,” amesema Musa na kuongeza:
“Sasa wewe ukimuona jirani yako anampiga mkewe kwa sababu amemfumania au anatembea nusu uchi na wewe utarudi nyumbani uanze kumpiga mkeo bila sababu eti kwa sababu tu jirani anampiga mkewe?”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF Mkoa wa Dodoma, Steven Chitema amesema chama hicho hakiungi mkono maandamano ya Chadema, kwani mpaka muda huu hawajapata ujumbe wowote kuhusu maandamano hayo kutoka ngazi ya juu.
Amesema chama hicho kina mfumo mzuri wa kupeana taarifa pale linapotokea jambo lakini mpaka sasa hawajapokea taarifa zozote kuhusu maandamano hayo.
Amewataka wanachama wa CUF kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2025 ili waweze kushiriki kikamilifu.
Naye Laila Tivuta kutoka chama cha ADC, amesema chama hicho kinaunga mkono maoni yaliyotolewa na viongozi wa kitaifa wa chama hicho kuhusu miswada iliyowasilishwa bungeni Novemba mwaka jana na wanaamini kamati itayafanyia kazi maoni yao waliyoyatoa bila kuyaacha.
Baraka Machumu kutoka chama cha Demokrasia Makini, amesema maoni yao kuhusu wakurugenzi na makatibu kata kutosimamia uchaguzi yazingatiwe kwani hawatendi haki katika kuwatangaza washindi na maandalizi hayo yaanze mapema kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa haujafanyika.
Hata hivyo jana, Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imewasilisha serikalini awamu ya kwanza ya rasimu ya uchambuzi wa sheria tatu za uchaguzi baada ya kupokea maoni kutoka kwa makundi mbalimbali.