Walimu wanne wa shule za msingi zilizopo Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza pamoja na mfanyabiashara mmoja mkazi wa Wilaya ya Nyamagana wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kughushi nyaraka za watumishi wa serikali ili kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifedha.
Akizungumza mkoani Mwanza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa ameeleza kuwa tukio hilo liliripotiwa kituo cha Polisi Misungwi Januari 4,2024 baada ya kugundua kwamba baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi wamesitishiwa makato ya mikopo yao wakati bado hawajamaliza kulipa madeni yao.
Baada ya ufuatiliaji Jeshi la Polisi liliweza kubaini kuwa nyaraka za kusitisha mikopo hiyo zilighushiwa na watumishi hao na kwenda kuomba mikopo mipya kwenye taasisi nyingine huku wakijua bado wanadaiwa marejesho kwenye taasisi walizokopa awali.
Watuhumiwa waliopanga na kuratibu njama za kughushi nyaraka kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia isiyo halali ni Majaliwa Philipo Mwaikambo,(34),mfanyabiashara na mkazi wa Nera Kata ya Isamilo ambaye ni mtuhumiwa sugu wa kughushi nyaraka.
Wengine ni Magreth Michael Simba (42), Mwalimu wa shule ya msingi Ntende Wilaya ya Misungwi,Mariam Ngwile (48),Mwalimu wa shule ya msingi Usagara Wilaya ya Misungwi, Beatus Nyombi,(53),Mwalimu wa shule ya msingi Mbalama Wilaya ya Misungwi na Jitashika Ezekiel Nchemba,(42),Mwalimu wa shule ya msingi Ntende Wilaya ya Misungwi.
Katika tukio jingine Mutafungwa ameeleza kuwa wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sugu wa usafirishaji na uuzaji wa dawa za kulevya ambao wamekuwa wakisafirisha kupitia barabara ya Mwanza – Musoma kwa kutumia magari binafsi.
Ambapo watuhumiwa hao ni Peter Charles kwa jina maarufu Peter Mirungi(50) mkazi wa Igoma, Said Abdallah (27),mkazi wa Igoma na Emenn Gamariel kwa jina maarufu Munuo (30),mkazi wa Igoma Wilaya ya Nyamagana.
Mutafungwa ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Januari 12,2024 majira ya saa 03:00 usiku katika Kijiji cha Ilungu, Kata ya Kahangala Wilaya ya Magu ambapo Askari Polisi wakiwa doria walifanikiwa kukamata magari mawili yakitokea Mkoa wa Simiyu na baada ya kusimamisha gari namba T.481 AJZ Toyota Surf lililokuwa likiendeshwa na Emenn Gamariel na lilipopekuliwa kulikutwa na vifurushi 17 vya dawa za kulevya aina ya Mirungi.
Wakati upekuzi ukiendelea ghafla lilitokea gari namba T. 406 EAM Toyota Alphard likiendeshwa na Said Abdallah akiwa na Peter Charles mmiliki wa mirungi hiyo.
“Baada ya mahojiano ilibainika kuwa gari namba T.406 EAM Toyota Alphard lilikuwa likisindikiza gari namba T. 481 AJZ Toyota Surf lililokuwa limebeba shehena ya Mirungi ili isikamatwe na Askari Polisi,”ameeleza Mutafungwa.
Watuhumiwa wote wamehojiwa kwa kina na watafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka pia litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahalifu.