Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2023, yakionyesha kuongezeka kwa ufaulu wa watahiniwa kwa asilimia 0.87 na ufaulu wa hisabati ukipanda kuliko masomo yote.
Mbali na kuongeza kwa kiwango cha ufaulu, ubora wa ufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu nacho kimeongezeka kwa asilimia 0.47 ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2022.
Akitangaza matokeo hayo leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Necta Dk Said Mohamed amesema asilimia 37.42 ya watahiniwa wamepata daraja la kwanza hadi la tatu ikilinganishwa na asilimia 36.95 waliopata madaraja hayo mwaka 2022.
“Jumla ya watahiniwa wa shule 471,427 kati ya 527,576 wenye matokeo ambao ni sawa na asilimia 89.36 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne.
Waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ni asilimia 37.42,” amesema Dk Mohamed. Kwenye matokeo hayo wapo watoto wa watu maarufu akiwemo Msemaji wa Yanga, Haji Manara ambaye kupitia mtandao wa Instagram ameandika;
"Well done My Young Boy Prince Hassan Haji, umeendelea kuipa heshma familia yetu na umenipa furaha sana Mwanangu, Ufaulu wako wa kidato cha nne umenipa mood nzuri,"
"Jana ilikuwa Siku nzuri sana kwangu,Nimemuoa Kipenzi changu Zaiylissa Buga, binti yangu Sayyidat Fatmah ilikuwa birthday na kidume kaniletea Division One ya ukweli,"
"Hongera Prince ila utambue ndio kwanza unaenda advance level (kidato cha tano na sita), safari yako ya kuisaka elimu ndio inaanza, nnalokuahidi ntakusomesha kwa kadri ntavyojaaliwa na nipo tayari kwa ajili yako ili utimize ndoto zako,"
Msanii wa Bongo Fleva, maarufu kama Baba Levo, amefurahishwa na matokeo ya kijana wake Levo, aliyepata one ya 13 kidato cha nne, akisifia kijana wake kafuata akili yake.
Kupitia mtandao wa kijamii Instagram, ameandika; "Hongera sana mwanangu Levo kwa kupata one ya 13 form four, umefata akili za mimi baba yako kabisa," mwisho wa kunukuu ambaye aliwahi kutamba na wimbo wake wa Ngongingo.
Kupitia mtandao huo wa Instagram, Dayna Nyange ameandika; "Ahsante sana mwanangu Rahma kwa ufaulu mzuri hakika mungu yu pamoja nasi, Dk Nyange mtarajiwa kabisaaa yaani leo I’m so so happy (nina furaha sana) and so proud of you my precious daughter Mungu akazidi kukutendea InshaAllah tukatimize malengo yetu, umenipa division one Kama ulivyo promise (ahidi) nakushukuru mama."