Wazee wa 5G Yanga Mzigoni Tena Leo, Ratiba ya Mechi Zote za Mapinduzi CUP Leo Hii Hapa
YANGA leo inarejea tena Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar kutafuta ushindi wake wa pili, baada ya juzi kuichapa Jamhuri mabao 5-0 kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi.
Yanga ndiyo inashikilia rekodi ya kutoa kipigo kikubwa kwenye michuano hiyo hadi sasa msimu huu, ukiwa ni mwendelezo wao wa kufunga mabao mengi kwenye mchezo mmoja.
Ilizichapa KMC, Simba, JKT Tanzania mabao matano kila moja kwenye Ligi Kuu Bara, lakini ikaichapa pia ASAS ya Djibout mabao 5-1 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo wa leo dhidi ya Jamus ya Sudan, ni mwendelezo mwingine wa mashabiki wa Yanga kusubiri kuona kile timu yao inaweza kufanya.
Katika mchezo wa kwanza wa Jamus, ilitoka sare ya bao 1-1 na KVZ, hivyo wanafahamu mchezo wa leo ndiyo umeshikilia hatima yao kama itapoteza basi itajiweka kwenye wakati mgumu wa kufuzu.
Jamus ambao walionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo wa kwanza, zaidi kwenye eneo la ulinzi, itatakiwa kufanya kazi kubwa leo saa 2:15 usiku kuhakikisha inawazuia washambuliaji wa Yanga ambao wanaonekana kuwa na uchu mkubwa wa kufunga.
Hata hivyo, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye hivi karibuni alisema anataka kuwatumia zaidi wachezaji waliokuwa hawatumiki kwenye Ligi Kuu Bara, anaweza kuendelea kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake na inaelezwa Agustine Okrah ambaye alitambulishwa juzi anaweza kuwemo kwenye kikosi hicho leo baada ya mchezo wa kwanza kuwatumia wachezaji wengi wazawa.
NGUSHI AANZA MAKALI
Katika mchezo wa kwanza, Crispin Ngushi ambaye kwenye ligi hana nafasi ya kucheza, alionyesha kiwango cha juu kwenye baada ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao.
Ngushi mbali na uwezo huo, aliwaonyesha pia mashabiki wa Yanga hana furaha hata akifunga baada ya kutoshangilia mabao yake yote mawili.
Hadi sasa huyu anaonekana ndiye mchezaji mwenye takwimu bora, akiwa tayari na mabao mawili na pasi moja ya bao na mwishoni mwa mchezo alitangazwa mchezaji bora, baada ya kuisaidia pia Yanga kuwa timu iliyofunga mabao mengi zaidi ikiwa imecheza mchezo mmoja tu.
“Hii ni nafasi ya wachezaji ambao hawapati nafasi kwenye ligi kuonyesha uwezo wao uwanjani ili kulishawishi benchi la ufundi,” alisema kocha msaidizi wa Yanga, Moussa N’Daw.
VITAL’O VS AZAM
Hii ni mechi nyingine ambayo mashabiki wanaisubiri kwa hamu kubwa. Baada ya Azam kukusanya pointi nne kwenye michezo miwili, sasa inakwenda kwenye mechi yenye maamuzi zaidi dhidi ya watoto wa Burundi, Vital’O.
Azam ambayo imeonyesha kiwango kizuri kwenye michezo miwili ya mwanzo, inatarajiwa kuingia tena uwanjani kuhakikisha inapata ushindi ili ifuzu moja kwa moja, lakini ikivaana na Vital O ambayo nayo haijapoteza mchezo hata mmoja kati ya miwili iliyocheza, ni lazima ipate ushindi ili kuwa na matumaini ya kufuzu hatua inayofuata.
Timu hizo za Kundi A, kila moja inaonekana kuwa ya moto, Azam inaongoza ikiwa na pointi nne baada ya michezo miwili, leo inakwenda kwenye mchezo wa mwisho wa kundi, huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Mlandege yenye pointi mbili sawa na Vital’O na nafasi ya mwisho ipo Chipukizi yenye pointi moja, hivyo mechi ya leo ndiyo imeshikilia hatima ya timu zinazoweza kwenda hatua ya robo fainali.