Waziri Aweso Agawa Pikipiki Zilizofungiwa Stoo Miaka Mitatu

 

Waziri Aweso Agawa Pikipiki Zilizofungiwa Stoo Miaka Mitatu

Hatimaye Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amegawa pikipiki 22 kwa Jumuiya ya Watumiaji Maji kwa Mkoa wa Lindi.


Pikipiki hizo zenye thamani ya Sh54 milioni zimegaiwa kufuatia ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani Lindi na kuhoji sababu ya kutotumika tangu ziliponunuliwa mwaka 2021 na kuiagiza Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kufuatilia suala hilo.


Kama hiyo haitoshi, Waziri Mkuu Majaliwa alimwagiza Waziri Aweso kumsimamisha kazi Ofisa Ununuzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Mkoa wa Lindi (Ruwasa), Kenedy Mbangwa.


Hata hivyo, kabla ya kusimamishwa kazi, Mbagwa alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia suala la vibali vya kutumia pikipiki hizo kutoka makao Makuu ya Ruwasa bila ya mafanikio.


Akizungumza jana Januari 25, 2024 wakati wa kugawa pikipiki hizo, Waziri Aweso amewataka Jumuiya ya Watumiaji Maji, kuzitumia kwa kazi iliyokusudiwa.


"Najua kuna watendaji walikuwa wanawakwamisha katika jumuiya zenu, ila niwaombe mwende mkafanye kazi iliyokusudiwa, Rais Samia (Suluhu Hassan) hataki wananchi wake wateseke kwa kukosa maji," amesema Waziri Aweso.


Aidha Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Muhibu Lubasa amesema kuwa pikipiki hizo 22 ni kwa ajili ya watumia maji wilaya zote.


Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia pikipiki hizo ili waende wakafanyie kazi.


Naye mmoja wa viongozi wa jumuiya hizo kutoka Wilaya ya Ruangwa, Ahmed Mwambe amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa pikipiki hizo alizosema zitawasaidia kuwafikia wananchi kirahisi.


"Tunamshukuru Rais Samia kwa kutupatia hizi pikipiki ili tuweze kumtua mama ndoo kichwani, tunaahidi kwenda kufanya kazi iliyokusudiwa," amesema Ahmed.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad