Yanga, KVZ mechi ya heshima





YANGA na KVZ zinarudi uwanjani usiku wa leo kuvaana kwenye mechi ya heshima ya kukamilisha ratiba ya Kundi B kwa timu hizo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, huku mapema watetezi, Mlandege watakuwa na kibarua kizito mbele ya Chipukizi kwenye mchezo mwingine wa kuhitimisha mechi za Kundi A.

Yanga ni kati ya timu nne zilizotangulia mapema robo fainali hadi sasa ikiwamo pia KVZ, Azam na Singida Fountain Gate ambayo usiku wa jana ilikuwa inamalizana na Simba kwenye mechi ya Kundi B, hivyo leo inashuka uwanjani ili kuhakikisha inamaliza kwenye nafasi ipi kwenye kundi ililopo.

Yanga ilifuzu juzi baada ya kuifunga Jamus ya Sudan Kusini kwa mabao 2-1 baada ya awali kuifumua Jamhuri kwa mabao 5-0, wakati KVZ imekusanya pointi nne kwa sasa ikiwa kwenye nafasi ya kumaliza ya pili ama ya tatu na kuingia robo kupitia kapu la mshindwa bora kwani pointi ilizonazo zinaibeba.

Kiuhalisi timu zote mbili zinakwenda kwenye mchezo huu kutafuta heshima ya kumaliza hatua ya makundi kileleni, kwani Yanga ikishinda itafikisha pointi tisa, na iwapo KVZ itashinda itamaliza ikiwa na pointi saba.

KVZ sio timu ya kubeza kwani ilianza michuano kwa kuifunga Jamhiri mabao 2-0 kisha kutoka sare ya 1-1 na Jamus, hivyo Yanga inapaswa kushuka uwanjani ikiwa makini, licha ya kuwa na uhakikisha wa kucheza robo fainali.

Yanga ndio timu inayoongoza kwa uwiano mzuri wa mabao ikifunga saba na kufungwa moja ikifuatiwa na Singida (hii ni kabla ya mechi ya jana) iliyofunga pia saba na kuruhusu mawili nyavuni mwake.

Kocha Gamondi ataendelea kumtegemea Crispin Ngushi mwenye mabao mawili kwenye eneo la mbele, wakati KVZ ikimtegemea kinara wake, Akram Omar ‘Haaland’ aliyefunga pia mabao mawili, lakini kubwa ni burudani ya soka wanayotarajiwa kupata mashabiki wa soka kwenye Uwanja wa Amaan katika mechi hiyo.


Mapema saa 10 jioni watetezi wa taji la michuano hiyo, Mlandege watashuka uwanjani kuvaana na Chipukizi katika mechi ya Kundi A ambayo ni mechi ya kisasi kwani timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa Ligi Kuu tya Zanzibar, Septemba 15 mwaka jana, Chipukizi ilifumuliwa bao 1-0 ikiwa nyumbani kisiwani Pemba.

Mlandege inahitaji ushindi ili iungane na Azam iliyofuzu robo fainali na iwapo itapoteza mbele ya Chipukizi yenye pointi moja itaifanya iliteme taji na kuipisha timu hiyo ya Pemba kwenda robo fainali.

Kocha wa Mlandege, Jalla Abdallah alisema amekiandaa vyema kikosi chake kuvuna pointi tatu katika mechi ya leo.

“Mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa kila timu inahitaji pointi tatu, lakini sisi tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunafuzu kucheza robo fainali,” alisema Jalla, huku kocha wa Chipukizi United, Mzee Ali Abdallah alisema pamoja na kikosi chake kuburuta mkia, bado kina nafasi ya kutinga robo fainali.

“Tutajipanga vizuri kuhakikisha tunashinda, mechi itakuwa ngumu kwa vile tunajuana, lakini jambo la msingi kwetu ni kuangalia tunapataje pointi tatu ili kukaa katika nafasi nzuri,” alisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad