Air Tanzania Wakanusha Ingine ya Ndege Kuwaka Moto, Watolewa Ufafanuzi Tukio Hilo



Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limesema tukio lililotokea katika ndege yake aina ya Airbus A220-300 iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda jijini Mbeya kupata hitilafu kwenye moja ya injini zake kuwa ni dogo na la kawaida.

Ndege ya shirika hilo namba 106 iliyoanza safari saa 12 jioni Jumamosi Februari 24, mwaka huu, ililazimika kukatisha safari na kurejea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya injini yake moja kupata hitilafu na kusababisha moshi ndani ya ndege.

"Kuna injini moja ilipata joto sana na ikawa na mafuta mengi ndiyo yaliyosababisha moshi ambao, uliingia kwenye mifumo ya hewa (AC) na ndiyo sababu moshi huo ukawafikia abiria sio ndege kuungua moto kama ilivyoelezwa," amesema Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Mhandisi Ladslaus Matindi alipozungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Februari 29, 2024 jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Mhandisi Matindi inakuja baada ya Mwananchi kuripoti tukio la injini ya ndege hiyo kupata hitilafu na kusababisha taharuki kwa abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo.

Baadhi ya abiria waliozungumza na Mwananchi, walieleza kuwa moshi huo ulisababisha taharuki, lakini baadaye marubani na wahudumu wa ndege walifanikiwa kudhibiti na hali kurejea kawaida.

Hata hivyo, ndege hiyo ililazimika kurejea Dar es Salaam na baada ya saa chache baadhi ya abiria waliendelea na safari huku wengine wakibadili tarehe ya safari.
Mhandisi Matindi amesema hali ndani ya ndege hiyo haikuwa ya kutisha na marubani na wahudumu wengine walichukua hatua za kiusalama kwa kuwapa taarifa abiria na kuwasihi kuwa watulivu na wasiwe na wasiwasi.

"Hali ya moshi ndani ya ndege ilidumu kwa dakika tano tu na ilichukua dakika 25 ndege kurudi Dar es Salaam na abiria walibadilishiwa ndege na 104 kati ya 122 waliendelea na safari huku 18 wakiomba kubadilishiwa siku ya safari," amesema Matindi.

Amesema suala la usalama kwa shirika hilo kwa abiria ndicho kipaumbele namba moja huku akisema endapo kungekuwa na majeruhi yeyote au abiria aliyeathirika kwa namna yoyote ile angepatiwa huduma za matibabu baada ya ndege kutua.


"Ni kweli hatukutoa taarifa mapema kuhusu tukio hilo kwa kuwa usafiri wa anga una taratibu zake, kuna tatizo dogo, kubwa na ajali. Mara nyingi kinachoripotiwa ni tatizo kubwa na ajali. Hatuwezi kutoa taarifa ya kila kitu hata tairi likiishiwa upepo," amesema Matindi.

Kuhusu ndege iliyohusika katika tukio hilo, Mhandisi Matindi amesema injini yake ndio ilikuwa imetoka kufanyiwa matengenezo kupitia kampuni ya Pratt & Whitney (PW) na tangu kurejea imeshafanya safari kwa saa 200 tu, hivyo kwa mujibu wa makubaliano itarejeshwa tena kwa matengenezo.

Alipoulizwa kuhusu abiria kuvaa maski wakati wa tukio hilo, Matindi amejibu kuwa, "Hakukuwa na abiria aliyevaa maski wala kuzimia kama ilivyoelezwa."


Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mhandisi Matindi aliambatana na Mkuu wa usalama wa ndege za ATCL, Emmanuel Tivai ambaye amesema jambo lililotokea ni la kawaida kwa vyombo vya usafiri na kwamba, cha muhimu ni hatua zinazochukuliwa baada ya hapo.

"Inapotokea tatizo kama hilo hatua kadhaa huchukuliwa ikiwa ni pamoja na kurudisha ndege uwanjani ili iangaliwe na wahandisi wake na hicho ndicho kilichofanyika," amesema Tivai.

Kwa upande wa wahudumu wa ndani ya ndege hiyo, walisema walidhibiti taharuki ndani ya ndege kutokana na mafunzo bora waliyonayo huku rubani msimamizi wa ndege za Airbus ndani ya ATCL, akisema hatua muhimu zilifuatwa katika tukio hilo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad