Ngereza amesema hayo kuelekea mchezo wa Jumamosi kati ya Yanga na Belouizdad ya Algeria ambao utapigwa katika dimba la Mkapa majira ya saa 1:00 jioni huku Yanga wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa kufungwa mabao 3-0.
Ngereza amesema CR wanahitaji sare tu ili kujiwekea mazingira mazuri ya kusonga mbele kuliko Yanga ambaye anahitaji ushindi katika mchezo huo muhimu kwao kabla ya kwenda kumalizana na vigogo Al Ahly.
"Kimahesabu timu zote kwenye kundi hili zina nafasi ya kwenda robo fainali, Yanga wanahitaji ushindi kwenye mechi hii ili wajiweke kwenye mazingira mazuri ya wao kufuzu robo fainali.
"Lakini Chabab Riadhi Belouizdad (CR Belouizdad) wao hata wakipata sare tu kwenye mchezo huu watakuwa wamejiweka kwenye mazingira mazuri. Kwanza watakuwa wameshaharibu mipango ya Yanga.
"Lakini pia watakuwa wamejiweka wao kwenye mazingira mazuri kwa sababu mchezo wa mwisho wanaenda kumaliza Medeama tofauti na Yanga ambao wao wanaenda kumaliza na Al Ahly ambayo ni timu ngumu sana. Kwa hiyo kwenye huu mchezo Yanga hawana namna nyingine zaidi ya ushindi tu," amesema Alex Ngereza.