TANZIA: Aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga SC, Imani Madega amefariki dunia asubuhi ya leo katika Hospitali ya Msoga iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Chalinze mkoani Pwani.
Akizungumza na #AzamTV mdogo wa marehemu, Beka Lenja amesema chanzo cha umauti wa mwanasheria huyo ni presha ambayo ilikuwa ikimsumbua.
Kutokana na kifo cha Madega, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wote walioguswa na msiba huo.
Madega alishika madaraka ya uwenyekiti pale Jangwani mnamo Mei 30, 2007 mpaka mwezi Agosti mwaka 2010.
Mbali na kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Madega pia aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA), na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF.
Madega atakumbukwa kwa misimamo yake ambapo kuna wakati aliwahi kusema kuwa Yanga inaweza kuishi kwa kutegemea viingilio pekee kwakuwa mashabiki walikuwa na hamasa kubwa ya kwenda uwanjani.