Binti Aliyepewa Cherehani Rais Samia Afunguka 'Niliomba tu Kwenye Comment ila Sikutegemea Ntajibiwa'



Binti huyu wa miaka 28 anajihusisha na ushonaji wa nguo, akiwa anamiliki eneo lake la biashara lililopo Kivule, jijini Dar es Salaam.


Misukosuko aliyemuandikia Samia ujumbe, nimedhulimiwa Sh85 milioni
Siku hiyo Rais Samia Suluhu Hassan kupitia ukurasa wake wa Instagram alitoa taarifa kuhusu ziara yake nchini Indonesia akielezea namna itakavyokuwa na tija na kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili.

Bila kujua atakachoandika kitasomwa au la, Beatrice akajibu chini ya andiko hilo la Rais akimtakia safari njema na kumuomba amletee zawadi ya cherehani.
Aliandika ujumbe uliosomeka: “Sawa mama. Ukiwa unarudi nyumbani naomba uniletee zawadi ya cherehani.”

Muda mfupi baadaye Rais Samia alijibu ujumbe wake na kumuambia. “Hujambo, Beatrice? Nimepata wasaa wa kuusoma ujumbe wako. Hongera kwa kazi na kujituma. Wasaidizi wangu watawasiliana na wewe kukusaidia upate mashine uliyoomba kwa shughuli zako. Nakutakia kila la kheri.”


Na hivyo ndivyo ilivyokuwa, Februari 4 ikiwa ni siku chache baada ya ahadi hiyo ya Rais wasaidizi wake walimtafuta Beatrice na akakabidhiwa cherehani nne.
Katika mahojiano aliyofanya na Mwananchi, Beatrice aliweka chapisho kujifurahisha na hakujua kama Rais ataujibu ujumbe wake.

Kitendo hicho cha mkuu wa nchi kujibu ujumbe wake kilimpa furaha ya aina yake na furaha hiyo iliongezeka maradufu baada ya kupokea mashine za kushonea kutoka kwake.

“Sikuwa na matarajio yoyote ya kujibiwa ujumbe nilioundika, ilitokea nimekaa nikaona ujumbe wa Rais kuhusu ziara yake nikajisema wacha leo nijibu na niombe cherehani kwa mama na kweli sikutegemea kama nitajibiwa, ukweli nimefurahi sana, ni kitu ambacho kimenipa furaha na 'motivation' (motisha) kwenye kazi zangu.

“Si hivyo tu, cherehani hizi zinanipa fursa ya kutoa ajira nne, sasa nitakuwa na jumla ya wafanyakazi 11, kwa kweli najivunia hatua hii, kila nikifikiria safari ya maisha niliyopitia hadi kufikia leo nina biashara yangu,” anasema Beatrice.


Hilo limetokea ikiwa ni mwaka mmoja tangu aanze kufanya shughuli zake nchini, kabla ya hapo miaka mitatu iliyopita alikuwa akishona nchini Japan.

Kama unafikiri kwenye suala la uthubutu Beatrice ameanzia kwa kutoa ombi lake kwa kiongozi mkuu wa nchi utakuwa umekosea, kwani binti huyu amekuwa na hali hiyo tangu utotoni na ndiyo imemfanya leo kuwa katika Jiji la Dar es Salaam.


Beatrice akionyesha baadhi ya cherehani alizopewa na rais
Harakati za upambanaji kwa binti huyu ambaye ni yatima zilianza baada ya kukatisha masomo akiwa kidato cha tatu, hili lilitokea baada ya ndugu zake kushindwa kumlipia ada ya Sh280,000 aliyokuwa anadaiwa.


Licha ya kuwa familia ilichangia yeye kuacha shule, alipochukua uamuzi huo hakuna ndugu aliyehitaji kuishi naye, hivyo akalazimika kuishi kwa marafiki akitangatanga huku na kule kutafuta msaada.

“Wazazi walifariki nikiwa mdogo, hivyo nikaanza kulelewa na bibi na babu, hata hivyo haikuchukua muda mrefu bibi naye akafariki na kubakia na babu ambaye mimi ndiyo namsaidia mpaka sasa. Ndugu walikuwa wananisomesha lakini baadaye ikaanza mivutano ya namna ya kunilipia ada, nikajikuta naacha shule,” anasema.

Wakati akiendelea kuhangaika akakutana na mtu aliyemsaidia Sh15,000, fedha ambayo aliitumia kama mtaji wa kuanzisha biashara ya mkaa na mafuta ya kupikia.

Licha ya kuwa biashara hiyo ilianza kumuingizia kiasi cha fedha ambacho kilimsaidia kuendesha maisha, Beatrice akajikuta anaingia kwenye mkumbo wa rafiki zake wa kuenda jijini Dar es Salaam kutafuta maisha.

Mwaka 2014 aliingia jijini Dar es Salaam kwa mara ya kwanza akitokea Tunduma, safari hiyo haikuwa ya kawaida, walilazimika kutumia usafiri wa lori ambalo pia waliomba lifti kwa dereva waliyekuwa wanafahamiana naye.

Mambo hayakuwa kama vile walivyotarajia, mwenyeji waliyemtegemea awapokee na wafikie alipokuwa anaishi hakuwapa ushirikiano, hivyo kukosa mwelekeo wa kuishi katika jiji hilo la kibiashara.

“Ilibidi tuanze kutafuta kazi itakayotuwezesha kuishi, ndipo tulipopata kazi ya kufua mashuka na kufanya usafi gesti kwa ujira wa kupewa sehemu ya kulala.

Tulianza kuishi maisha ya kushirikiana kwa kila kitu kuanzia malazi hadi mavazi na nguo za ndani, jambo lililokuwa linahatarisha afya zetu, lakini kutokana na hali tuliyokuwa nayo ilitulazimu kufanya hivyo,” anasema Beatrice.

Hakuridhishwa na maisha hayo, hivyo akatafuta kazi ya uhudumu wa baa iliyomwezesha kuongeza kipato chake na kufanikiwa kupanga chumba Magomeni.

Huko akakutana na marafiki wapya ambao walikuwa na uhusiano na wanaume wa Kizungu, wakamshawishi ahudhurie sherehe ambayo ingemwezesha na yeye kupata mwanaume wa kigeni.

Bila kusita Beatrice alifuata ushauri huo na akapata mwanamume aliyekuwa anafanya kazi ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania, huyu ndiye aliyeanza kubadilisha maisha yake.

“Ni kweli nilimpata mwanamume, sikuwa naweza kuzungumza Kiingereza ila tulielewana na tukaanzisha uhusiano. Baada ya muda yule mwanamume akatakiwa arudi Japan akaniambia niambatane naye.

“Sikuwa na sababu za kupingana na hilo, nilienda naye na kwa pamoja tukaanza maisha mapya Japan, hata hivyo yule mwanamume alikuwa na wivu mno kiasi hakutaka nifanye shughuli yoyote ya kuniingizia kipato. Nilivumilia kwa muda, ikafika wakati nikachoka, ikabidi nimuombe ruhusa ya kurudi Tanzania naye akaridhia,” anasema.

Hata hivyo, Beatrice hakurudi nyumbani kama alivyoaga, bali alikwenda kuishi kwa marafiki aliowapata akiwa nchini humo na kuanza maisha mapya.

Uamuzi huo ulikuwa na matokeo chanya kwake, kwani muda mfupi baada ya kuondoka kwa mwanamume huyo alipata kazi kwenye mgahawa na akapata dili la kuonyesha mavazi yaliyokuwa yanaandaliwa na wabunifu mbalimbali.

Kuwa karibu na wabunifu kukampa wazo la kujifunza kushona, ndipo alipoanza kujifunza kupitia mtandao wa Youtube akiangalia hatua kwa hatua ushonaji wa nguo unavyofanyika.

Bado aliendelea na kazi yake ya uhudumu kwenye mgahawa, kazi hiyo ilimwezesha kukutana na mpenzi ambaye baada ya kuanzisha naye uhusiano na kugundua anajifunza kushona alivutiwa zaidi na kazi hiyo na kumshawishi aachane na uhudumu ajikite kwenye ushonaji.

“Haikuwa rahisi kushawishika niache kazi na yeye aligundua hilo, hivyo akaniambia nimtajie kiasi cha mshahara ninacholipwa kwenye mgahawa na akanilipa mishahara ya miaka mitatu ili niachane na kazi hiyo, nijikite na ushonaji.

“Alinipatia Dola 72,000 (Sh183.2 milioni) na alininunulia mashine ya kisasa ya kushonea, hakuishia hapo, kwa kuwa yeye ni mwenyeji alianza kunitafutia wateja, hapo ndipo safari yangu ya ubunifu na ushonaji ilipoanzia,” anasema Beatrice.

Akaendelea kushona nguo na wakati mwingine kushona mikoba, huku akiendelea kuishi na mwanamume huyo ambaye anamchukulia kama mume wake, licha ya kuwa hawajafunga ndoa.

Licha ya kuwa maisha yake kwa kiasi kikubwa yapo Japan, Novemba mwaka jana Beatrice aliona ipo haja ya kuifanya biashara yake Tanzania ili iweze kuwahudumia wanafamilia wake waliopo nchini, akiwemo babu na wadogo zake.

Ushauri kwa vijana na jamii

Kama bahati ya mtende iliangukia kwake basi inaweza kutokea kwa mwingine, hivi ndivyo anavyoamini Beatrice, hivyo anawataka wanajamii kuwa na matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii.

Msisitizo wake kwa vijana ni kuhakikisha wanapata elimu na kuachana na mawazo ya kukimbilia maisha kama ambavyo ilitokea kwake na kujikuta akiingia kwenye mambo yasiyofaa.

“Niliishia kidato cha tatu kutokana na changamoto ambazo zilikuwa nje ya uwezo wangu, lakini kwa sasa elimu ni bure, nawashauri watoto na vijana kushika elimu ili kupata maarifa ya kufikia ndoto zao,” amesema.

“Vijana hawana sababu, wasikurupukie maisha kwa sababu dunia ya leo mambo yamekuwa mengi, hasa ukatili wa kingono, hii ni kutokana na watu kutumia nafasi ya shida aliyokuwa nayo mtu kutimiza haja zake,” anasema na kuongeza:
“Pia kwa wale watu wanaotaka kwenda nje ya nchi kutafuta maisha bila kuwa na kipaji au msaada wa uhakika nawasihi wasifanye hivyo, kwa kuwa kuna matukio ya unyanyasaji ughaibuni.”

Beatrice pia anashauri jamii kuweka hamasa kubwa kwenye somo la stadi za kazi na kupewa kipaumbele shuleni ili watoto waweze kujengewa ubunifu, kupunguza changamoto ya upatikanaji wa ajira nchini.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad