Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), David Misime, amesema jeshi hilo linatoa onyo kwa watu wanaojichukulia sheria mkononi na kuwataka waache kufanya hivyo, kwani ni kinyume cha sheria na ukiukwaji wa misingi ya haki za binadamu.
Ametolea mfano wa matukio mbalimbali ya wananchi kujichukulia sheria mkononi ikiwemo la jana mkoani Tanga katika wilaya ya Korogwe, eneo la Msambiazi, ambapo waendesha bodaboda waliteketeza kwa moto basi la Kampuni ya Sai Baba linalofanya safari zake Dar es Salaam na Arusha baada ya basi hilo kumgonga dereva wa bodaboda ambaye alifariki dunia.
Pia amesema Februari 2, mwaka huu mkoani Manyara, wilayani Babati wananchi walifanya vurugu na kufunga barabara, wakishinikiza Jeshi la Polisi liwakabidhi mtuhumiwa aliyekuwa akituhumiwa kumbaka kisha kumuua mtoto wa miaka saba.
Amesema polisi inaendelea kuwasaka wale wote waliohusika na uhalifu huo wa kuchoma basi wilayani Korogwe, ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.