Bondia Hassan Mwakinyo Ashuka Viwango Tanzania



Bondia Hassan Mwakinyo ameng’oka kwenye orodha ya mabondia watatu bora (Top 3) wa muda wote Tanzania. Pia bondia huyo ameporomoka na kushindwa kupenya kwenye 10 bora (Top 10) wa Tanzania kwa mabondia bora wa muda wote.


Bondia huyo aliyewahi kuingia kwenye tatu bora, ameporomoka kwenye viwango hivyo, huku, wakongwe Rogers Mtagwa, Rashid Matumla na Mbwana Matumla wakitajwa kwenye tatubora.


Kwa mujibu wa Mtandao wa Ngumi za Kulipwa wa Dunia (Boxrec), mabondia wa sasa wanne pekee ndio wameingia kwenye top 10 ya ubora wa muda wote huku wakongwe ni sita.


Mabondia wanaopigana hadi sasa waliotajwa kwenye ubora “pound for pound’ ya Tanzania kwa muda wote ni Fadhil Majiha anayekamata nafasi ya nne, Ibrahim Class (ya tano) , Antony Mathias (ya sita) na Juma Fundi aliyekamata nafasi ya 10.


Mwakinyo ambaye kwa muda mrefu alikuwa kwenye tatu bora akiwavutia kasi ‘kaka zake’ Mtagwa na Matumla ameporomoka hadi nafasi ya 11. Tangu 2018 alipomchapa Sam Eggington kwa Technical Knock Out (TKO) nchini Uingereza, bondia huyo alikusanya pointi zilizompandisha na kuingia kwenye orodha ya mabondia bora wa muda wote wa Tanzania akiwa sanjari na wwkongwe hao waliokuwa vinara wa muda wote.


Tangu wakati huo, Mwakinyo alikuwa akipambana kuifikia na hata kuipita rekodi ya vinara wa muda wote, wakongwe Rogers Mtagwa na Rashid Matumla aliye nafasi ya pili bila mafanikio hadi hivi karibuni alipoporomoka na kushindwa kufika rekodi ya Wakongwe hao waliostaafu ambao wameendelea kukalia usukani.


Mkongwe mwingine, Mbwana Matumla ametajwa kwenye nafasi ya tatu. Vinara hao watakumbukwa kwa uwezo wao wa kutwaa mataji enzi wakizichapa, ambapo Matumla au Snake boy kama alivyopenda kujiita, kabla ya kustaafu mwaka 2013, alikuwa ametwaa ubingwa wa dunia Mara tatu mfululizo.


Tangu 1993 alipoingia kwenye ngumi zakulipwa amepigana mapambano 72, ameshinda mara 49, amepigwa mara 19 na sare nne. Mtagwa ambaye baada ya kustaafu mwaka 2014 alikwenda kuishi Marekani aliingia kwenye ndondi mwaka 1997, amewahi kuwa bingwa wa dunia wa WBO kwa vijana na WBC, hadi anastaafu alipigana mapambano 47, ameshinda 27.



Mbwana Matumla bondia pekee Mtanzania aliyewahi kuingia kwenye rada za promota maarufu wa ngumi dunia, Don King aliwahi kuwa kwenye tatu bora ya dunia enzi zake.


Hadi anastaafu 2017, bingwa huyo wa zamani wa IBO Afrika alikuwa amepigana mara 29 na kushinda mapambano saba, miongoni mwa mapambano yaliyompa umaarufu ni lile la 1998 alipomchapa KO ya raundi ya kwanza, Tamas Szkallas kwenye ukumbi wa Diamond Jubillee, Dar es Salaam.


Jingine ni lile alipigana Venezuela mwaka 2000 alipokwenda kuzichapa na Eddison Torres, pambano ambalo lilimkutanisha na Don King kwa mara ya kwanza na kumtaka kwenye promosheni yake ya ndondi.



Mwakinyo ambaye ametwaa ubingwa wa WBO Afrika hivi karibuni hajaweza kutwaa mataji makubwa ya dunia, huku kukaa muda mrefu bila kupigana pia kukichangia kumporomosha kwenye renki.


Pambano lake gumu la mwisho lilikuwa mwaka 2022 alipochapwa kwa TKO na Liam Smith wa Uingereza huku lile la Eggington mwaka 2018 likimpaisha kidunia hadi nafasi ya 14 kwenye uzani wake wa awali wa super welter (hivi sasa amehamia kwenye uzani wa middle) kabla ya kuanza kuporomoka taratibu hadi sasa ni wa 89 duniani kwenye uzani wake na kwenye ubora wa muda wote Tanzania aking’oka nafasi ya tatu hadi ya 11.


Bondia mwingine, Francis Miyeyusho licha ya kukomaa kwenye gemu tangu 1998 hadi sasa, ameonyesha utofauti kwa ‘vijana’ kwa kuwa wa saba kwenye orodha ya mabondia bora wa muda wote wa Tanzania.


Wakati nyota wengine waliotamba miaka ya 1980, Hamisi Kimanga na Joseph Marwa wakitajwa kwenye nafasi ya nane na tisa. Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) Chaurembo Palasa amesema kupanda au kushuka kwenye renki inategemea na kiwango cha mpinzani wako.


“Huwezi kupanda kwa kupigana na yoyote tu hata uwe unapigania ubingwa wa nini, kama mpinzani wako hana kiwango ni ngumu kukupandisha kama ambavyo utapigana na mwenye kiwango bora.


“Ndio sababu tunaona kwenye ubora wa muda wote wale mabondia ambao hawapigani baadhi wameendelea kuwa ni bora hadi sasa sababu ya aina ya mapambano waliocheza wakati wao.”


Hata hivyo Palasa alishauri mabondia wa sasa kupigana na wapinzani wenye viwango. “Hasa hawa mabondia wetu wakubwa, wacheze na wenye viwango ili wawapandishe, hilo sasa ni jukumu la menejimenti ya bondia na mchezaji.


“Changamoto ni kwamba mapromota wengi wa Tanzania hawana mabondia, hivyo menejimenti za mabondia zina wajibu wa kukaa na oromota na kukubaliana bondia wa kupigana naye awe wa kiwango gani kwa kuangalia atamuongezea nini bondia wao kwenye renki,”alisema.


Mwakinyo kwa upande wake amesema malengo yake ni mikanda, ndio sababu ameendelea kupigania mikanda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri. “Watu watakumbuka, niliwahi kufikisha hadi nyota nne na nusu, lakini hazikunisaidia, huko duniani wanaangalia mikanda zaidi, ndio sababu nimejikita huko,” amesema bondia huyo.


Promota wa ngumi, Shomari Kimbau alisema kinachoendelea kuwabeba mabondia wa zamani kwenye renki ni mapambano waliyopigana, aina ya mikanda na ubora wa mabondia waliocheza nao wakati huo.


“Wale wa zamani hawakuchagua mechi, walikuwa wakipigana tu, ndio sababu tunaona rekodi zao zimeendelea kuwa bora. Hawa wa sasa wengi wao wanachungulia mechi, wanachagua sana wapinzani, wakiona ni wakali wengi wao wanawakataa, tofauti na zamani walikuwa wakipigana tu.


“Pia miaka ya karibuni hakukuwa na promota anaye mshikilia bondia, kama zamani tuliwashikilia na kuwaendeleza, walipigana mapambano makubwa ya ubingwa, kuanzia wa Tanzania, Afrika Mashariki na kati, Afrika, Mabara na hata dunia, hivi sasa ndio tumeanza kurudi polepole hivyo tutakaa sawa tena.”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad