Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Lowassa, huku akimuelezea alikuwa kiongozi shupavu, mwanaharakati hodari na alikuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko ya kisiasa.
Lowassa alifariki dunia jana Jumamosi, Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu.
Katika ujumbe wake alioutoa kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo X (zamani Twitter), Mbowe amesema; "Lowassa alikuwa kiongozi shupavu, mwanasiasa mahiri, mwanaharakati hodari na alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini.
“Alikuwa rafiki yangu na mshirika katika safari ya kuleta demokrasia ya kweli Tanzania. Alikuwa mtu mwenye hekima, busara, ujasiri, uzalendo, mtu mwenye huruma, upendo na msamaha kwa wote. Alikuwa mtu mwenye maono, mipango na mtekelezaji mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
“Kwa niaba ya Chadema na Watanzania wenzangu, napenda kutoa salamu zangu za dhati za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wapenda demokrasia wote kwa kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa, kilichotokea Februari 10, 2024.”