Baadhi ya mashabiki na wachambuzi wa soka wamekuwa wakisema kuwa, ni wakati wa Simba kuachana na Chama umefika. Kwanini? Kwa sababu kiwango chake kinaelekea ukingoni. Hana maajabu makubwa tena kama zamani.
Wengine wanapenda kutumia kauli ya kuwa ‘Chama huyu sio yule’. Kila mtu amesema la kwake. Maneno yalikuwa mengi zaidi baada ya Simba kumsimamisha Chama kutokana na madai ya kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu. Hapa ndipo wengine walitilia mkazo kuwa ni wakati sahihi wa pande hizo mbili kuachana.
Wakati baadhi ya wadau wa soka wakiamini hivyo, Chama alijumuishwa kwenye kikosi cha mwisho cha Zambia kilichoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zilizofanyika Ivory Coast.
Hii ina maana kuwa, wakati Tanzania tukiamini Chama amekwisha, Zambia wanaamini kuwa bado ana kitu. Ndio sababu alijumuishwa kwenye kikosi cha nyota 27 wa Afcon na alikiwasha vile vile. Utakataa nini wakati kwenye mechi na Stars, alitokea benchi la kuitibulia Tanzania kwa kona iliyozaa bao la kusawazisha na kufanya mechi iishe ya sare?
Ikamrejesha kambini mapema kwa ajili ya ratiba ngumu ya mechi za Ligi Kuu Bara. Simba ilikuwa na mechi tano za ligi ndani ya siku 12 tu. Ni ratiba ngumu kweli kweli.
Ratiba ngumu kama hii inahitaji timu yenye kikosi imara sana. Bahati mbaya hadi Ligi inarejea Simba ilikuwa imekaa kambini kwa siku tatu tu. Haikuwa imefanya maandalizi makubwa.
Ndio nyakati hizi Chama amekwenda kuwakumbusha mashabiki ubora wake. Amekiwasha kwelikweli. Kwenye mchezo dhidi ya Tabora United mambo yalionekana mepesi kutokana na kiwango bora cha Chama siku hiyo. Aliwafanya mabeki wa Tabora United kile alichojisikia.
Alitengeneza nafasi za hatari kwa kadri Simba ilivyokuwa ikishambulia. Alikuwa katika dunia yake. Tena alifanya hayo katika uwanja usiovutia wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Vipi mchezo dhidi ya Azam FC? Ilikuwa ni mechi ngumu kwa Simba. Walizidiwa kila kitu katika kipindi cha kwanza. Wakaruhusu bao la mapema. Azam walikuwa bora sana japo walikosa umakini wa kutosha kuimaliza mechi.
Mambo yakawa magumu kwa Simba katika kipindi cha pili Azam FC walipoamua kurudi nyuma na kujilinda. Mianya ya kufunga ikawa migumu kuonekana.
Hata hivyo, nini kilitokea? Chama aliwakumbusha tena wana Simba thamani ya miguu yake. Akafunga bao la kulazimisha katika dakika za jioni. Akainusuru Simba na kipigo kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Ndivyo wachezaji wakubwa hufanya. Huonekana katika nyakati ngumu. Ni kama Chama alivyofanya dhidi ya Azam. Simba ilikuwa na mechi ngumu zaidi dhidi ya JKT Tanzania majuzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kwanini ilikuwa mechi ngumu? Kwanza Simba ilikua imetoka kucheza mechi mfululizo. Wachezaji wamechoka. Benchi la ufundi limechoka. Kila mmoja amechoka.
Ni katika nyakati za ratiba kama hiyo kocha msaidizi, Selemani Matola naye akafungiwa mechi tatu. Pili, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Simba kucheza kwenye Uwanja wa Isamuhyo. Tena dhidi ya JKT Tanzania ambayo msimu huu imekuwa kwenye kiwango bora.
Hata hivyo, mechi hii iliamuliwa kwa bao la Chama. Ndizo nyakati hizi ambazo Chama huwakumbusha mashabiki wa soka uwezo wake. Anajibu kwa vitendo.
Anajibu kwa kuamua mechi. Anawakumbusha kwa kuwatetemesha wapinzani. Ni kweli kwamba Simba inapaswa kufikiria maisha baada ya Chama, lakini tusipotoshe kwa madai kuwa Chama amechoka. Mwamba wa Lusaka bado yupo kwenye ubora wake.
Bado ana miaka michache ya kuendelea kusumbua. Bado ana muda wa kuendelea kuonyesha makeke yake. Ila wakati akiendelea kufanya hivyo, Simba inapaswa kusaka wachezaji mahiri zaidi wa kuibeba baada ya Chama.
Ila kama Simba watafanya kosa la kuachana na Chama hivi karibuni, sitashangaa kumuona akisajiliwa na timu nyingine kubwa nchini. Tena akaenda kufanya makubwa katika timu hiyo. Mwisho wa siku watalaumiwa viongozi kwa uamuzi ambao siyo wa busara.