BAO la jioonii dakika ya 90 la kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama limeiokoa timu hiyo na kichapo kwenye Dabi ya Mzizima ambayo imepigwa leo katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Chama ambaye amekuwa na kiwango kizuri katika mechi tatu za hivi karibuni tangu klabu yake imsamehe, amefunga bao hilo kwa mpira wa adhabu ya kutengwa nje ya eneo la 18 ambao umezama moja kwa moja nyavuni na kumwacha kipa wa Azam, Mohamed Mustafa akishangaa.
Bao hilo limeibua shangwe dimbani hapo huku mashabiki waliokuwa wameshakata tamaa na kutoka uwanjani wakirudi na kusherehekea, huku likiwaacha na mshangao Azam FC, wakiwa wameshajiandaa kushangilia kuondoka na pointi tatu ndani ya CCM Kirumba.
Azam imetangulia kupata bao mapema kipindi cha kwanza dakika ya 14 kupitia kwa Prince Dube 'Mwanamfalme' aliyemalizia vyema krosi ya Paschal Msindo kutoka upande wa kushoto. Msindo alipokea mpira huo kutoka kwa beki wa kati, Mkolombia, Yeison Fuentes. Bao hilo limedumu kwa dakika 90 kabla ya Chama kutibua furaha hiyo dakika za nyongeza.
Dube ameendelea kuifunga Simba katika michezo ya Dabi ya Mzizima, kwani msimu uliopita alifunga kwenye mchezo wa Ligi Kuu na kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam na kuitupa nje kwenye mashindano hayo, Simba.
Bao la Dube limetibua pia mwendo wa Simba wa kutopoteza mchezo katika mechi zake za viporo na iliifunga Mashujaa 1-0, ikaichapa Tabora United mabao 4-0 na keshokutwa Simba itarejea tena CCM Kirumba kumenyana na Geita Gold, huku Azam ikiikaribisha Geita Gold Februari 16.
Sare hiyo ni ya kwanza kwa Azam tangu ilipofungwa na Namungo FC mabao 3-1 katika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam Oktoba 27, 2023 na imecheza michezo sita na kushinda yote.
Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikah ameendelea kutopoteza mchezo wa Ligi Kuu Bara tangu alipotua kuchukua nafasi ya Mbrazil, Robertinho na kocha huyo raia wa Algeria katika mechi zake tano za ligi hiyo ameshinda tatu na sare mbili, alizifunga Tabora United 4-0, Mashujaa 1-0, Kagera Sugar 3-0, KMC 2-2 na Azam FC 1-1.
Simba imefikisha alama 30 na kuendelea kubakia katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi huku Azam ikifikisha pointi 32 katika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga wenye alama 37 kileleni ambao wameweka pengo la pointi saba dhidi ya Simba na tano kwa Azam.
DAKIKA 45 NGUMU KWA SIMBA
Kipindi cha kwanza Simba imekosa utulivu kwenye eneo la ulinzi na ushambuliaji na kujikuta ikipoteza mipira mingi zikiwemo krosi ndefu, huku wenzao Azam wamecheza kwa mipango licha ya kutoshambulia sana lakini imekuwa hatari mara zote ikifika langoni mwa Simba.
Moja ya madhaifu yaliyoonyeshwa na Simba ni eneo la ulinzi ambalo halikucheza kwa maelewano hasa kipindi cha kwanza, jambo ambalo huenda limechangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya kikosi yaliyofanywa na Kocha Benchikah.
Eneo la kulia, wanakocheza beki Hussein Kazi na Israel Mwenda badala ya Kennedy Juma na Shomari Kapombe limeonekana kutokuwa na maelewano na kusababisha kupitika kirahisi, kukosa utulivu, na wakati mwingine kupoteza mipira muhimu, likiwemo bao la kwanza la Azam lililofungwa na Prince Dube krosi ikitokea upande wao.
Licha ya kufunga mchezo uliopita dhidi ya Tabora United, mshambuliaji mpya wa Simba, Fredy Michael bado hajamudu vyema nafasi hiyo kuweza kuwasahaulisha Wana Simba, John Bocco, Jean Baleke ama Moses Phiri. Nyota huyo hakuwa na makali yoyote kwenye mchezo huo akikosa baadhi ya nafasi muhimu na kuamsha hasira za mashabiki jukwaani.
Kutokana na udhaifu huo, benchi la ufundi la Simba limelazimika kufanya mabadiliko ya mapema kipindi cha pili dakika ya 46, wakitoka Israel Mwenda, Hussein Kazi na Fredy Michael na kuwapisha Shomari Kapombe, Kenedy Juma na mshambuliaji, Pa Jobe. Azam nao wakimtoa Yahya Zayd na kumwingiza beki, Daniel Amoah ili kuimarisha eneo la ulinzi na kulinda bao lao.
Timu hizo zimefanya mabadiliko mengine kipindi cha pili, Simba ikiwapumzisha Fabrice Ngoma na Saido Ntibazonkiza dakika ya 68 na 77 na kuingia Mzamiru Yassin na Luis Miquissone, huku Azam ikiwapumzisha Paschal Msindo, Djibril Sylla, Feisal Salum na Prince Dube na kuingia Kipre Jr, Cheikh Sidibe, Franklin Navaro na Ayoub Lyanga dakika ya 76 na 80.
WAKOLOMBIA WAWEKA REKODI, MUSTAFA FRESHI
Mastaa wapya wa Azam FC waliosajiliwa dirisha dogo, Kipa, Mohamed Mustafa kutoka El Merreikh ya Sudan na Beki wa kati, Yeison Fuentes kutoka Colombia wameanza katika mchezo huo na kumfanya Mkolombia huyo kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Colombia kucheza Ligi Kuu Bara ambayo ni namba sita kwa ubora barani Afrika.
Fuentes ameanza katika mchezo huo na kutengeneza beki pacha na Yannick Bangala akimweka benchi beki raia ya Ghana, Daniel Amoah, huku kipa, Mustafa akianza pia na kumweka benchi, Zuberi Foba.
Kwa dakika 90 alizocheza Mkolombia huyo amekuwa na utulivu mkubwa wa akili na akiwa na mpira kwani amezima baadhi ya mashambulizi na kutoa pasi muhimu, dakika ya pili aliokoa hatari ya Chama lakini dakika ya nne akapoteza mpira mbele ya Michael Fredy japokuwa wenzake wakamsaidia kuondoa hatari hiyo.
Beki huyo ndiye aliyehusika kwenye bao la Azam dakika ya 14, akipiga mpira mrefu kwenda kwa Msindo aliyetoa pasi iliyomaliziwa vyema na Dube.
Kipa, Mustafa ameonyesha umakini na utulivu mkubwa langoni kwa dakika zote 90 akiokoa michomo kadhaa na kuiweka timu yake sehemu salama huku akipata kashikashi baada ya kugongana na mastraika wa Simba na kulazimika kutibiwa mara kadhaa, miongoni mwa 'save' alizofanya ni shuti la Kibu Denis dakika ya sita, mpira wa kutengwa wa Chama dakika ya 13, krosi hatari ya Israel Mwenda dakika ya 36 na ile ya Kibu dakika ya 39.
Mkolombia mwingine, Franklin Navaro anayecheza nafasi ya ushambuliaji naye ameweka rekodi ya mchezaji kutoka taifa hilo kucheza Ligi Kuu Bara na amecheza kwa dakika 10 baada ya kuingia kipindi cha pili dakika ya 80 akichukua nafasi ya Feisal Salum.
MABADILIKO 4,5
Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikah aliendelea kufanya mabadiliko katika kikosi chake na kuhakikisha kila mchezaji anapata nafasi ya kucheza, huku akiwapumzisha wengine kusubiri mchezo wa Jumatatu dhidi ya Geita Gold.
Katika mchezo wa leo, Benchikah amefanya mabadiliko ya wachezaji wanne walioanza mchezo wa Jumatano dhidi ya Tabora United, na aliwaanzisha Israel Mwenda, Hussein Kazi, Fabrice Ngoma na Fredy Michael wakichukua nafasi za Shomari Kapombe, Kennedy Juma, Sadio Kanoute na Pa Jobe.
Kwa upande wa Azam FC, nao walifanya mabadiliko ya wachezaji watano kutoka kwenye kikosi kilichopata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa mwisho wa ligi.
Azam imewaanzisha kipa mpya, Mohamed Mustafa, Yannick Bangala, Yeison Fuentes, Sylla na Abdul Sopu wakichukua nafasi za Zuberi Foba, Edward Manyama, Iddi Nado, Kipre Jr na Daniel Amoah.
Simba: Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Hussein Kazi, Che Fondo Malone, Babacar Sarr, Kibu Denis, Fabrice Ngoma, Fredy Michael, Saido Ntibazonkiza na Clatous Chama
Azam: Mohamed Mustafa, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yannick Bangala, Yeison Fuentes, James Akaminko, Yahya Zayd, Sylla, Prince Dube, Feisal Salum na Abdul Sopu.