CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemlilia kada wake, Thadei Ole Mushi, aliyefariki dunia jana tarehe 4 Februari 2024, akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Salamu za rambirambi za CCM zimetolewa leo tarehe 5 Februari 2024 na idara yake ya itikadi, uenezi na mafunzo.
“CCM kimepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa ya msiba wa ndugu Thadei Ole Mushi, kilichotokea tarehe 4 Februari 2024 akiwa kwenye matibabu hospitalini jijini Dar es Salaam. Uongozi wa CCM chini ya mwenyekiti ndugu Dk. Samia Suluhu Hassan, unatoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu jamaa na marafiki,” imesema taarifa hiyo.
Chama hicho kimesema kitamkumbuka marehemu Mushi kwa umahiri wake na uthubutu wa kukosoa bila woga.
“CCM kitamkumbuka kwa umahiri na uzalendo wa taifa lake, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na alitumia maarifa na karama yake kutoa maoni na hisia zake katika nyanja nyingi za kijamii, kisiasa na kiuchumi. Alikuwa kiongoni mwa vijana wachache wenye uthubutu, alisimamia alichokiamini hakuona soni kukosoa wala kukosolewa,” imesema taarifa hiyo.