“Kuelekea mwisho wa msimu na Chama atakuwa anamaliza mkataba wake Simba, je Wekundu wa Msimbazi watakuwa tayari kupambana na vigogo wengine kumpa Chama mkataba mpya? Hili ni swali gumu. Kuna ugumu mwingi hapa. Baada ya kutokuamini Chama kwa muda mrefu bado Simba watatakiwa mezani kukaa naye kumuongezea mkataba. Sio kitu rahisi sana. Inawezekana Chama mwenyewe akawa ana hisia za Simba si wenzake tena kwa yote waliyotenda ikiwemo kumfungia.
Simba wakiamua kumuongezea mkataba Chama bado vita itakuwa ngumu pia. Kuna watani watakuwa wanasubiri kumuunganisha Chama na Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki na Maxi Nzengeli. Kwa sasa wanaweza kujifanya hawataki lakini ni wazi kama kuna klabu imewahi kumtamani Chama DUNIANI basi Yanga inaongoza. Wanamtaka kwa sababu mbili. Wanaamini katika ubora wake, lakini pili wanataka tu kuwaumiza. Mchezaji kipenzi anapokatiza mtaa mmoja kutoka Msimbazi kwenda Jangwani basi roho huwa kwatu maradufu kwa watani ambao wanakuwa wameshinda vita.
Lakini katika umri wake, ukiachana na kupenda kushangiliwa na mashabiki wa hizi timu, Chama anataka pesa. Kuna Azam wanaangalia pambano hili wakiwa na noti za kutosha. Kama hautaamini kuhusu noti zao basi kamuulize ni kipi kilibadilisha akili za Fei Toto akaamua kuondoka Jangwani kwenda Mbande kule Chamazi.” — Edo Kumwembe