Edo Kumwembe "Inachekesha Sana Eti Inonga Hauzwi"



Ni wazi moja kwa moja jicho la mawakala na klabu kubwa za ndani ya Afrika limekwenda kwa Inonga. Tofauti yake na Diarra ambaye tunaamini labda kimo kinamdhibiti katika nafasi yake, Inonga ni beki wa kati ambaye ni mrefu, ana nguvu na ana kasi.

Kifupi, ana sifa zote za kucheza katika zile klabu za Afrika Kaskazini. Angeweza kuwa na sifa zote za kucheza hata Ulaya kama angekuwa na miaka 20. Katika hili soko la ndani kuna wababe wenye pesa chafu ambao wanaweza kufanya lolote na muda wowote. Nimecheka kusikia kauli ya kiongozi wa Simba, Inonga hauzwi.

Rais wa Real Madrid, Florentino Perez aliwahi kutuambia hakuna mchezaji asiyeuzwa duniani. Inategemea tu una kiasi gani cha pesa. Hawa rafiki zetu matajiri wa Afrika kina Pyramids, Al Ahly, Waydad, Zamalek, Berkane, FAR Rabat na wengineo wana pesa chafu. Wenyewe kwa wenyewe wanaweza kutunishiana misuli lakini sio klabu ya Afrika Mashariki ikitunishiana nao misuli.

Wanaweza kuweka Dola 500,000 lakini Simba wakaguna na kuweka kifua. Baadaye wakubwa wanakutana tena katika kikosi cha kahawa wanaweka mezani Dola 800,000 bado Simba wanatunisha misuli. Wakirudi na ofa ya Dola 1 milioni sioni kama Simba wanaweza kuzuia. Ukiandika kwa Dola kuna watu wanaweza wasielewe lakini Dola 1 milioni ni zaidi ya Sh2.2 bilioni.

Unadhani Yanga walitamani kuachana na Mayele? Unadhani Simba walitamani kuachana na Clatous Chama na Luis Miquissone wakati ule? Ukweli, wachezaji wetu wote wanauzwa. Ni suala la kufika bei fulani tu. Kitu kizuri hata mashabiki wa siku hizi ni waelewa. Wanajua soka ni biashara na kuna bei huwa haikataliki. Tuendelee tu kuwaandaa kisaikolojia wachezaji wetu wote wapo sokoni isipokuwa kwa bei sahihi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad