Marcus Rashford amekua kwa kulelewa na mama yake tu. Alimshuhudia mama yake, mrembo Melanie akifanya vibarua kwenye sehemu tatu tofauti ili kupata pesa za kumhudumia yeye pamoja na ndugu zake, kaka na dada.
Wakati mwingine Malanie alikuwa hali ili kufanya chakula kitoshe kwa watoto wake, ambapo nyakati nyingine walihitaji chakula cha bure kutoka kwenye shule ili kuhakikisha Marcus na ndugu zake wanne, walau wanapata sahani moja ya chakula kwa siku. Maisha hayakuwa matamu.
Miaka 20 baadaye, Rashford kwa sasa analipwa Pauni 325,000 kwa wiki huko Manchester United, lakini anagundua kwamba pesa si kila kitu, baada ya mwanzoni kudhani kwamba angekuwa nazo angemaliza matatizo ya familia yake. Lakini, badala yake, straika huyo wa England, pesa zinamweka kwenye matatizo makubwa.
Mapema wiki iliyopita, Rashford alikumbana na adhabu ya faini ya Pauni 650,000 kutoka kwenye klabu yake baada ya kukesha baa na kushindwa kuhudhuria mazoezi. Awali, Rashford aliidanganya klabu yake kwamba anaumwa baada ya kupiga simu kusema hivyo, lakini mitandao ya kijamii ilimuumbua baada ya kuposti picha alizokuwa akikesha kwenye kumbi ya starehe ya usiku.
Akawekwa kikao na kocha wake Erik ten Hag pamoja na mkurugenzi wa michezo wa Man United, John Murtough, Jumatatu iliyopita na kinachosemwa, Rashford aliwaambia, amepoteza hamu ya kucheza soka.
Maisha yake binafsi pia yamekuwa na majanga mengi, matatizo ambayo anayahamishia hadi uwanjani.
Kinachoelezwa ni kwamba Rashford amekuwa mtu wa kupenda familia yake, lakini huko ndiko linakoanzia tatizo na kumwaathiri kwa kiasi kikubwa kwenye mambo yake ya uwanja.
Chanzo kilifichua: “Marcus siku zote amekuwa mtu wa familia. Kaka zake ndiyo mawakala wake na washauri pia, lakini ukweli huko ndiko shida zinakoanzia. Amekuwa na dili nyingi za udhamini, zinazompa uwezo mkubwa wa kununua nyumba na majumba, huku akilipwa mishahara mikubwa,kwa kifupi ni tajiri mtoto.
"Amejiweka kwenye nafasi ya kuiweka sawa familia yake kifedha, lakini hicho sicho kinachotokea. Kumekuwa na malumbano makubwa juu ya masuala ya pesa yeye na mawakala wake kwa miezi kadhaa sasa, mambo si mazuri. Marcus haelewi kabisa. Hafahamu ni nani wa kumwaamini na hilo limemfanya hadi uwezo wake wa uwanjani kupungua.”
Kaka zake Rashford, Dwaine na Dane, ndiyo mawakala wake, washauri wake wa kibiashara na watunza pesa.
Wote wanaishi kwenye mitaa ya kitajiri, Wilmslow, Cheshire, sambamba na mama yao Melanie.
Wanavyoishi sasa, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma walipokuwa Withington, Manchester, wakati wanakua.
Tatizo lilianzia kwenye familia baada ya Dane, 31, kupatwa na tatizo huko Miami, Oktoba mwaka jana. Alikuwa na kesi, lakini baadaye ilifutwa, lakini athari zake ni kubwa. Dwaine alilazimika kuiweka sokoni nyumba yake baada ya kuamini kwamba usalama wake haupo tena kufuatia polisi wa Miami kubainisha anwani hiyo kutokana na kesi ya Dane. Na tangu wakati huo, inaelezwa, Dwaine, 40, na Marcus hawapo kwenye mazungumzo mazuri licha ya kwamba amekuwa akisimamia baadhi ya masuala ya mdogo wake.
Rashford amekuwa akiendelea pia kuishi na marafiki zake wa utotoni, lakini wengine wameshindwa kulinda utu huo, kwa kuchukua kadi za benki za mchezaji huyo na kwenda kufanya manunuzi ya vitu vya thamani kubwa bila ya ridhaa yake.
Wanamfanya kuwa na msongo wa mawazo na wala hawajali kwa maana ya kumzuia kwenda kwenye mambo ya starehe, kulewa na kucheza kamari.
Kingine kinachomsumbua Rashford ni mpenzi wake wa tangu enzi za shule, mrembo Lucia Loi, waliyeachana kwenye majira ya kiangazi mwaka jana.
Uhusiano wao ulikufa baada ya Rashford kupigwa picha akiwa anaingia hotelini huko Miami akiwa na mwanamke mwingine saa 11 alfajiri. Lucia ameachana na Rashford, lakini mwanamume huyo bado anampenda mrembo Lucia kwa kuwa ndiye anayeamini wanapendana kweli, kwa sababu walianza akiwa hana kitu, tofauti na hawa wa sasa, ambao anaamini wanahitaji pesa zake tu.
Chanzo kilibainisha: “Marcus ana makabati yamejaa nguo za wabunifu mbalimbali, saa na vidani vya thamani, lakini alikutana na Lucia wakati akiwa hana kitu kabisa. Anajua alimpenda yeye kama yeye, sio pesa. Kwa sasa Rashford anahisi wanawake anaokutana nao kwa sababu tu wanavutiwa na pesa.”
Kutaka kusaidia kila mtu kwenye familia yake pia ni kitu kingine kinachomsababisha matatizo Rashford.
Rashford ameruhusu majumba yake mengi sana kuishi ndugu zake, akimfanya mama yake kuwa msimamizi.
“Marcus anafanya kila anachoweza kusaidia watu,” kilibainisha chanzo hicho.
Hivi karibuni alishindwa kwenda kuhudhuria mazishi ya ndugu yake kwa kuhofia kwamba angekuwa kwenye wakati mgumu wa kuombwa pesa.