NYOTA wa zamani wa Yanga, Feisal Salum na Fiston Mayele ni kama wamepishana na gari la mshahara. Unaambiwa tangu waondoke Jangwani mambo yamezidi kuwanyookea Wananchi, huku kibao cha mafanikio viwanjani kikionekana kuwageuka.
Yanga ni kama imeendelea pale ambapo iliishia msimu uliopita licha ya kuwapoteza wachezaji hao ambapo mmoja, Feisal, alitua Azam na Mayele akienda Pyramids FC ya Misri, na timu hiyo ilifanya mabadiliko katika benchi la ufundi kwa kumleta kocha Miguel Gamondi ili kurithi mikoba ya Nasreddine Nabi imekuwa moto wa kuotea mbali.
Gamondi ambaye aliongezewa nguvu katika maeneo mbalimbali ukiwa ni mpango wa kuboresha kikosi ameifanya Yanga kuutafuna mfupa ambao ulimshinda Nabi kutinga hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kama haitoshi ameifanya kutinga hatua ya robo fainali ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Al Ahly.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa Yanga na mashabiki wake ambao wanafurahia mwenendo wa timu na kusahau kabisa kama kwenye kikosi walikuwa na Mayele pamoja na Fesail, ambao waliwafanya msimu uliopita kutembea vifua mbele, lakini hali ni tete kwa wachezaji hao katika michuano ya kimataifa.
Feisal mwenye mabao tisa katika Ligi Kuu Bara akiwa na Azam FC, aliishia raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika aakiwa na Azam ambapo walitolewa na Bahir Dar Kenema ya Ethiopia kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 kwenye matokeo ya jumla licha ya awali kuonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuvuka hatua hiyo kutokana na ugeni wa wapinzani wao kwenye michuano hiyo.
Kwa upande wake, Mayele ambaye alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita sambamba na Saido Ntibazonkiza wakiwa na mabao 17, ameishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Pyramids FC baada ya wikiendi iliyopita kuchapwa na TP Mazembe ya kwao DR Congo kwa mabao 3-0.
Licha ya kusalia mchezo mmoja mbele kwenye kundi A, Pyramids yenye pointi nne hata kama itashinda mchezo wa mwisho katika hatua hiyo dhidi ya Nouadhibou ya Mauritania haiwezi kufikia pointi 10 ilizonazo Mamelodi Sundowns na TP Mazembe.
Msimu uliopita Mayele alikuwa mfungaji bora pia upande wa Kombe la Shirikisho Afrika akipachika mabao manane na kuifanya Yanga kutinga fainali ambako ilipoteza kwa kanuni ya bao la ugenini mbele ya USM Alger.
Kwa upande Feisal hakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kwenye michezo ya mwishoni mwa msimu baada ya kuwa katika mvutano na waajiri wake hao wa zamani kutokana na sababu za kimaslahi.