Licha ya timu yake kukata tiketi ya kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku ikiwa na mechi moja mkononi, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema hawezi kusema ameridhika kwa kuwa kazi haijaisha hadi lengo lao litimie kwenye michuano hiyo ya kimataifa ikiwa ni pamoja na ushindi dhidi ya Al Ahly.
Wiki iliyopita Yanga ilikata tiketi hiyo baada ya kuifunga CR Belouizdad mabao 4-0, hivyo kuungana na Al Ahly ya Misri kuwa timu zilizofuzu hatua ya robo fainali kutoka Kundi D.
Hata hivyo, Al Ahly na Yanga zitakutana Ijumaa wiki hii nchini Misri kuhitimisha mechi zao za hatua ya makundi, lakini pia mchezo huo ndio utakaoamua timu itakayoongoza kundi lao.
Yanga yenye pointi nane inahitaji ushindi ili kuongoza kundi hilo, wakati Al Ahly ambayo ipo kileleni ikiwa na alama tisa, yenyewe ikihitaji sare yoyote ama ushindi ili kuhitimisha hapo ilipo.
Kikosi cha Yanga kimeondoka jana jioni kuelekea nchini Misri kwenye mchezo wao huo wa mwisho katika hatua ya makundi kikiwa na matarajio makubwa ya kupata ushindi.
Akizungumza nasi jana, Kocha Gamondi amesema anaifahamu vizuri Al Ahly na ana kazi kubwa ya kupata ushindi katika mchezo huo ili kuongeza hali ya kujiamini.
Amesema kila mchezaji yupo tayari kuona wanaendelea kuwa kwenye ubora na wanakwenda katika mchezo huo kusaka ushindi licha ya kutambua ubora wa wapinzani wao hao.
“Kila mmoja anapenda kuona wachezaji wanapata matokeo na uzuri ni kwamba wanajituma na kutimiza majukumu yao kwenye mechi ambazo tunacheza na kutaka matokeo.
"Ni furaha tumefuzu kucheza robo fainali ambayo tulikuwa tunaitafuta kwa miaka mingi, lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Al Ahly,” amesema Gamondi.
Naye Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema timu imeondoka jana saa 11:55 jioni kuelekea Misri kwa Shirika la Ndege la Ethiopia ambapo walitarajia kufika Ethiopia saa 2:33 usiku na kisha kuwasili Misri saa saba usiku.
“Tunaenda na msafara wa watu 60 na ambao umegawanyika katika makundi matatu; wachezaji 24, benchi la ufundi 13 na watendaji wakuu na maofisa wa klabu 23. Tunatambua ni mchezo muhimu na wenye ushindani mkubwa kulingana na ubora wa mpinzani wetu, hivyo tumejiandaa vizuri,” amesema Kamwe.