Mkurugenzi Mtendaji wa Manara TV, Haji Manara amesema kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wanapaswa kumfukuza Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Adel Amrouche kutokana na vitendo vyake viovu ikiwa ni pamoja na kuihujumu klabu ya Yanga kuelekea mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya CR Belouizdad.
kauli hiyo ya Manara imekuja ikiwa ni muda mfupi baada ya waandishi wa Manara TV kumfumania kocha huyo akiwapokea wapinzani wa Yanga, CR Belouizdad katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuketi nao Serena Hotel akiwapa mawili matatu kuhusu Yanga na Tanzania kwa ujumla jambo ambalo limetafsriwa kuwa ni kulihujumu Taifa.
Waandishi hao baada ya kumfata ili wafanye nae mahojiano aligoma na hata baada ya kumpiga picha aliwakamata na kuzifuta picha hizo kwenye simu zao huku akiwaonya kuwa iwapo watampiga picha tena atawachukulia hatua za kisheria.
“Pamoja na Ualgeria wake, yeye ni Kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, kwa nini ashiriki kuihujumu Timu inayotoka ya Tanzania? Sawa klabu inayocheza ni ya Tanzania na inacheza na timu kutoka Algeria, na yeye ni Mualgeria, alipaswa aweke Ualgeria wake pembeni, nadhani TFF wanapaswa kufanya jambo.
“Kumekuwa na tuhuma nyingi sana juu ya huyu kocha, mengine tunayafumba tu kwa sababu ya maslahi ya Timu ya Taifa. Kuna mambo mengi nimeyasikia na mengine kutoka kwa wachezaji wa Taifa Stars aliyoyafanya na anayoendelea kuyafanya kwa timu yetu, tuliacha kwa sababu Stars ilikuwa inashiriki AFCON.
“Lakini hili analolifanya kwa Yanga na ni timu ambayo inawakilisha nchi ya Tanzania, dhidi ya timu ya nchi yake (CR Belouizdad) wakati yeye ni kocha wa Timu ya Taifa ya Tanzania, analikosea heshima Taifa. Pale Serena kuna kamera za CCTV kila mahali, Airport ni kamera za CCTV kila eneo, wafanye uchunguzi, ni kitendo cha dakika moja tu TFF wakaomba ushahidi Serena na Airport watapewa tangu alipoingia mpaka anondoka.
“Na kama itabainika kuwa huyu anayefanya haya ni Kocha wa Taifa Stars, basi TFF wamchukulie hatua, na hatua ya kwanza ni kumfukuza tu. Kocha wa aina hii ni kumfukuza tu wala sio kumfuga. Abaki na Ualgeria wake atuachie Taifa Stars yetu. Kama anasema atachukua hatua na sisi tutatumia wanasheria wetu nini cha kufanya.
“Kocha analetwa hapa analipwa na Serikali lakini anashiriki kuihujumu Yanga na Taifa, hatuwezi kufuga hawa watu. Kocha mwenyewe haeleweki timu inacheza vipi, pata umpatae, mechi ikichezwa hujui utafungwa saa ngapi, kocha wa nini huyu, aende kwao tu.
“Timu ya Yanga inayocheza kuna wachezaji wa Timu ya Taifa na pengine kuna wachezaji wengine ambao yeye anatakiwa awatazame ili awaongeze kwenye kikosi chake. Hawa makocha ndio wanaosababisha Timua ya Taifa inapocheza watu wanashindwa kuishabikia kwa sababu ya mambo ya hovyo wanayoyafanya,” amesema Manara.
Ikumbukwe kuwa, Amrocuhe amesimamisha na TFF kuinoa taifa Stars baada ya kutoa kauli za kichochezi kati ya Tanzania dhidi ya Taifa la Morocco wakati wa AFCON akidai kuwa CAF imekuwa ikilipendelea taifa hilo.
Yanga wanatarajia kuingia Dimbani Jumamosi, Februari 24, 2024 katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad huku wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 3-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Agleria mwishoni mwa mwaka jana.