Juzi Simba imemalizana na JKT Tanzania na sasa Henock Inonga atahusika kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast itakayopigwa Uwanja wa Felix Houphouet Boigny, Abdjan nchini humo Februari 23, 2024.
Jambo jema kwa Simba beki huyo atakuwa mwenyeji wao kwenye mechi dhidi ya Asec kwani anaujua vyema uwanja wao wa nyumbani (Felix Houphouet Boigny) kwa sababu timu yake ya DR Congo ndipo iliagia mashindano ya Afcon baada ya kutolewa na Afrika Kusini.
Kurejea kwa Inonga ndani ya kikosi cha Simba kutampa jeuri kocha mkuu wa chama hilo, Abdelhak Benchikha kwani kabla ya kuondoka alikuwa akicheza kama beki kiongozi huku akiwa chaguo la kwanza kwenye nafasi ya beki wa kati akicheza sambamba na Mcameroon, Che Malone Fondoh.
Hata hivyo pengo la Inonga halikuonekana moja kwa moja kwenye kikosi cha Simba tangu ameondoka kwani katika mechi nne timu hiyo ilizocheza imeruhusu bao moja tu katika sare ya 1-1 vna Azam lakini nyingine tatu dhidi ya Mashujaa (1-0), Tabora United (4-0), na Geita Gold (1-0), imetoka na hati safi ‘Cleansheets’.
Katika mechi hiyo, Simba inahitaji zaidi ushindi ili kurejesha matumaini ya kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokea kundi B, linaloongozwa na Asec yenye alama 10, ikifuatia Simba yenye pointi tano, kisha Jwaneng Galaxy yenye alama nne na Wydad Casablanca inayoburuza mkia na pointi tatu kila timu ikiwa imecheza mechi nne.
Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo mbili ulipigwa uwanja wa Benjamin Mkapa Novemba 25 mwaka huu na Simba ikiwa mwenyeji ikalazimishwa sare ya mabao 1-1, bao la Mnyama likiwekwa dakika ya 44 na Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ kwa mkwaju wa Penalti na Asec kusawazisha dakika ya 77 kupitia kwa Serge Pokou.