Kampuni ya Precision Air Matatani, Yadaiwa Shilingi Bilioni 65



Dar es Salaam. Kampuni ya Export Development Canada (EDC) imefungua kesi Mahakama Kuu ya Uingereza, ikilishtaki Shirika la Ndege la Precision kudai Dola26 milioni za Marekani (Sh65 bilioni) zilizotokana na makubaliano kwenye mauziano na ukopeshaji wa ndege.

Kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa hiyo, mwishoni mwa mwaka wa 2012, kampuni ya Canadian Export Credit Agency (ECA) ilitoa ufadhili wa moja kwa moja wa kuiwezesha Precision Air, kununua ndege mbili aina ya ATR42-600 kutoka kwa mtengenezaji wa Kifaransa na Italia.

Inadaiwa kuwa, mkataba maalumu wa ukodishwaji ambao anayekodi anakuwa kama mmiliki, ulihusu uwezekano wa ndege hizo kuwa kama dhamana kwa niaba ya EDC.

Precision Air ilikuwa na jukumu la kulipa kodi kwa ndege hizo, baada ya muda, umiliki halali wa ndege ungehamishwa mara mkopo utakapoisha.

Lakini nyaraka zilizowasilishwa Mahakama Kuu ya Uingereza Desemba, zilionyesha kuwa shirika hilo lilishindwa kulipa EDC kwa mujibu wa mkataba wa kukodisha na haikujibu maombi kadhaa ya malipo tangu mwaka 2021.

Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa Precision Air, Hillary Mremi, alipoulizwa, amekiri suala hilo lakini hakutaka kutoa maoni zaidi.

"Uongozi unajua, tunafanyia kazi suala hilo. Lakini kwa sasa hatupo tayari kutoa maoni zaidi," amesema Mremi.

EDC inadai Dola 13 milioni za Marekani (Sh32.5 bilioni) chini ya mkataba wa kukodisha ndege ya kwanza, inayojumuisha deni la Dola 11.7 milioni (Sh39.3 bilioni) na Dola 1.3 milioni (Sh3.25 bilioni) kama fidia.


Kwa ndege ya pili, EDC inadai karibu Dola 11.3 milioni (Sh28.25 bilioni) kama deni na Dola milioni 1.6 (Sh4 bilioni) kama fidia. Jumla ya deni hilo ni wastani wa Sh65 bilioni.

Katika taarifa yake ya kifedha iliyo sainiwa Septemba 2022, Precision Air ilisema ndege hizo kwa kiasi kikubwa hazikuwa zikifanya kazi na shirika lilikuwa katika mchakato wa kurejesha ndege hizo kwa mkopeshaji.

"Ndege hizi zimekuwa hazifanyi safari tangu mwaka wa 2017 kutokana na matatizo ya kiufundi, hazihusiki tena ratiba ya ndege zetu," imeeleza hiyo.


Msemaji wa EDC alikataa kutoa maoni alipoulizwa kuhusu mahali zilipo ndege hizo mbili za ATR.

"Kwa sasa, tuna vizuizi vingi katika kile tunachoweza kuwashirikisha," alisema.

Mkataba huo pia uliimarisha mpango wa Precision Air wa kuboresha ndege zake na tovuti ya kampuni bado zinaendelea kuonyesha kuwa lilikuwa shirika la kwanza duniani kutumia ndege za ATR 42-600.

Precision Air iliundwa mwaka 1993 na inahudumia maeneo mbalimbali Tanzania, Kenya, na Visiwa vya Komoro. Sehemu kubwa ya hisa zake asilimia 41 inamilikiwa na Kenya Airways.

Katika miaka ya hivi karibuni, shirika hilo Afrika Mashariki limekumbana na changamoto za kifedha pamoja na malalamiko juu ya huduma na tukio kubwa la hivi karibuni ni ajali ya ndege yao aina ya ATR42 iliyoua watu 19, Novemba mwaka jana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad