Kocha wa Yanga Miguel Gamondi, amesema ameridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na mastaa wake kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC, juzi.
Yanga juzi, ilivaana na KMC kwenye mchezo wa Ligi uliopigwa Uwanja wa Jamhuri Morogoro na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 na kuendelea kutawala kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 43.
Baada ya ushindi huo, Gamondi alitoa tamko kwamba kiwango ambacho timu yake imekionyesha ni cha juu na ndicho alichokuwa anataka kukiona kwenye michezo yote msimu huu.
Gamondi raia wa Argentina, alisema licha ya ushindi huo bado timu yake ilikuwa inaweza kufunga mabao mengi zaidi kama washambuliaji wake wangekuwa na utulivu kila wanapofika langoni.
"Hiki ndio kiwango ambacho tulikuwa nacho kabla ya ligi haijasimama, naona tunaanza kurejea kule ambako tulitoka kwenye kiwango kizuri na kupata mabao bila shida, tunatakiwa kuwa na njaa ya ushindi kama hivi ambavyo tumecheza," alisema Gamondi.
"Nawaheshimu sana wapinzani wetu, narudia hii (KMC) ni timu ambayo inanivutia inavyocheza kwa kuwa wachezaji wake wanajiamini sana lakini kama tungekuwa na utulivu tungeweza kushinda zaidi ya mabao haya, kitu muhimu tunatakiwa kuendeleza hapa tulipo leo," alisema.
Baada ya mchezo huo wa juzi kinara wa ufungaji kwenye ligi Stephane Aziz Ki akiwa na mabao 10, alionekana hakufurahia kutolewa uwanjani, ambapo Gamondi alisema ameshazungumza naye na kuweka kila kitu sawa.
"Hakuna tatizo lolote, Aziz alitaka aendelee kubaki uwanjani ili afunge zaidi, ni sawa lakini sisi tuliona kitu zaidi ya hapo jambo zuri ni kwamba yuko sawa, nimezungumza naye na kila kitu kipo sawasawa."
Kesho mabingwa hao watetezi watakuwa uwanjani kuvaana na Polisi Tanzania mchezo wa mtoano wa Kombe la Azam Shirikisho hatua ya 32 bora, kabla ya kuvaana na CR Belouizdad kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi wikiendi ijayo.