Kocha Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta amesema Arsenal ni lazima iwe kwenye mjadala linapokuja suala la kusajili mchezaji supastaa wa aina ya Kylian Mbappe.
Mshambuliaji huyo wa Paris Saint-Germain kwa muda mrefu amekuwa akizungumzwa kutaka kuachana na miamba hiyo ya Ufaransa na hilo linaweza kutimia mwishoni mwa msimu huu.
Hata hivyo, bado hakuna uhakika wa asilimi zote ni wapi Mbappe hasa atakwenda mwishoni mwa msimu huu baada ya sasa kudaiwa atakwenda Real Madrid.
Los Blancos bado inapewa nafasi kubwa ya kunasa saini yake, lakini Liverpool nayo inamhitaji Mbappe huku Kocha wa Arsenal Arteta akisema kitu, “hilo linaweza kujadiliwa”.
Arteta, ambaye kikosi chake hii leo kitachuana na Burnley kwenye mchezo wa Ligi Kuu England amesema: “Inapotokea kuwapo na mchezaji wa kariba kama hiyo siku zote tumekuwa na mazungumzo. Lakini, kama mnavyosema, hii kitu inaweza kuwa kwenye mtazamo tofauti.”
Real Madrid bado inaonekana kushika usukani kwenye mbio za kumfukuzia mshambuliaji huyo licha ya Arsenal kudaiwa Mbappe anaweza kuchagua kwenda huko ili tu, akapite njia alizopita shujaa wake, Thierry Henry, ambaye pia alichezea AS Monaco kama Mbappe.
Hata kama gharama za kumudu huduma ya Mbappe zipo juu, Arteta anataka timu yake isikae kinyonge na badala vake itazame namna ya kuonyesha uwepo wao katika vita ya kunasa mchezaji mkubwa kama huyo.
Arsenal ikifanikiwa kunasa saini ya Mbappe basi huenda ikafanikiwa kutengua kitendawili cha kubeba mataji makubwa kwenye Ligi Kuu England na pengine Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa maana ya kuwa na timu itakayokuwa imnejitosheleza kiushindani.