Wanigeria wanaoishi Afrika Kusini wameshauriwa kuwa waangalifu sana kuelekea mechi ya nusu fainali ya AFCON 2023 kati ya Super Eagles na Bafana Bafana mnamo Jumatano, Februari 7.
Katika taarifa yake siku ya Jumanne asubuhi, Kamisheni Kuu ya Nigeria yenye makao yake makuu mjini Pretoria, Afrika Kusini iliwataka raia wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi kuwa makini na lugha wanayotumia kabla na baada ya mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu na ghamu na kuwataka kuwa makini kuhusu mahali ambapo watachagua kutazama mchezo huo. .
Raia wa Nigeria katika nchi hiyo ya Afrika Kusini waliombwa zaidi kuepuka sherehe kubwa na uchochezi endapo Super Eagles watawashinda Bafana Bafana.
“Kamisheni Kuu inashauri raia wa Nigeria kuwa makini na matamshi yao, wawe makini na wapi wanachagua kutazama mechi, hasa katika maeneo ya umma na wajiepushe na sherehe za sauti, ghasia au za uchochezi iwapo Super Eagles watashinda mechi, ” Ubalozi wa Nigeria ulisema katika taarifa.
Taarifa hiyo ilisomeka zaidi, " Zaidi ya hayo, Wanigeria wanapaswa kudumisha mwenendo mzuri wanaojulikana nao, na kuwa watiifu wa sheria kabla, wakati na baada ya mechi. Ikitokea chokochoko zozote zisirudishwe bali ziripotiwe kwa mamlaka husika.”
Ubalozi ulieleza kuwa tahadhari hiyo inafuatia vitisho vingi vinavyotolewa dhidi ya Wanigeria wanaoishi Afrika Kusini iwapo Bafana Bafana itashindwa na Super Eagles Jumatano usiku.
Timu hizo mbili kali za Afrika zitamenyana mwendo wa saa mbili usiku wa Jumatano, ili kubaini ni nani atafuzu kwa fainali za AFCON 2023.