Paul Makonda, Mbowe na Lema |
Lema Afunguka Sababu ya Kukataa Kusalimiana na PAUL Makonda Msiba wa Lowassa
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Godbless Lema ametaja sababu iliyomfanya kutosalimiana na Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa Paul Makonda walipokutana kwenye msiba wa Waziri Mkuu mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa mapema jana, Jumamosi Februari 17.2024 Ngarash, wilaya ya Monduli, mkoani Arusha kuwa ni uwepo wa nidhamu chafu ya kada huyo wa CCM inayoenda sambamba na kuchafua majina ya watu.
Akizungumza na wanahabari msibani hapo Lema amesema Makonda amekuwa akitumia muda mwingi kuchafua watu kwa kuwapa tuhuma wasizostahili kwenye majukwaa tofauti lakini pale anapokutana na watu hao anaigiza uwepo wa urafiki miongoni mwao jambo ambalo Lema analipinga badala yake amepanga kuwashawishi viongozi wenzake ndani ya chama hicho wamuunge mkono msimamo wake wa kutoshirikiana na Makonda.
"Nitaongea hata na viongozi wenzangu, hakuna mtu mwenye nidhamu chafu kama Makonda, anapita Barabarani anatukana watu, anadhalilisha watu halafu anakuja kwenye sehemu kuna kusanyiko la jamii anafikiri maisha ni rahisi tu, kwamba mtu anaweza kukuita mwizi, anaweza kukuita kwamba unauza madawa ya kulevya, anaweza akasema umekula sadaka, anaweza akakutamkia jambo lolote, anadhalilisha watu Barabarani, anatukana watu Barabarani halafu anakuja kwenye cycle kama hizi anataka kujifanya kwamba mtu wa watu, Kwa hiyo mimi siwezi kusalimiananaye" -Lema.
Akizungumzia msiba wa Lowassa Lema ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini amesema kwa muda mrefu amekuwa na mahusiano binafsi ya kifamilia kati yake na watoto wa Lowassa hivyo anamfahamu kama miongoni mwa watu watulivu na kwamba ameshirikiana vyakutosha wakati Lowassa alipojiunga na CHADEMA 2015 ambapo aligombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho.
Amesema hana uhakika wa moja kwa moja kama Lowassa alirejea CCM kutoka CHADEMA kwa mapenzi yake binafsi, badala yake anadai kuwa kilichomrejesha ni uwepo wa mazingira yasiyokuwa rafiki ya kisiasa wakati huo ambayo pia yalisababisha yeye (Lema) na viongozi wengine wa upinzani kuikimbia nchi yao.