Mahakama Yaigomea Vodacom Kesi ya Tangazo iliyofunguliwa na Msanii


Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imekataa maombi ya kampuni ya Vodacom iliyoomba mahakama iondoe amri ya kutupilia mbali maelezo yake ya utetezi wa maandishi kwenye kesi ya ukiukaji wa mkataba wa tangazo la kibiashara iliyofunguliwa dhidi yake na mwanamitindo, Hadija Mweta.

Tangazo hilo ni la Red Relax maarufu kama Please Call me.

Hadija amefungua kesi ya madai dhidi ya Vodacom na kampuni ya Aggrey & Clifford Ltd, iliyokuwa wakala wa Vodacom katika mchakato na mkataba wa tangazo hilo, pamoja na mambo mengine, akidai fidia ya Sh1 bilioni, riba na gharama za kesi.

Katika tangazo hilo Vodacom inawaeleza wateja wake na jamii kwa ujumla kuwa wasiteseke kwa vifurushi visivyoaminika vya kupiga simu, intaneti, kutuma ujumbe wa maneno na hivyo huwaalika kununua au kujiunga kwenye kifurushi cha red relax kupitia au kwa kupiga menu iliyowekwa.

Hadija anadai makubaliano yalikuwa tangazo hilo lilikuwa ni kwa ajili ya runinga pekee na kwa kipindi cha siku 30 tu, lakini Vodacom imesambaza katika mitandao yake ya kijamii kama vile youtube, facebook na iliendelea kulitangaza kwa miaka mitano bila malipo wala makubaliano mapya.

Machi 9, 2023, kesi hiyo ya madai namba 114/2022 ilipoitwa kwa ajili ya kikao cha kwanza cha majadiliano ya namna ya uendeshaji kesi hiyo, Vodacom haikufika mahakamani.

Mahakama iliamuru kuondolewa kwa maelezo ya utetezi wake wa maandishi, iliyokuwa imeyawasilisha mahakamani hapo kama majibu ya awali dhidi ya madai ya mdai katika kesi hiyo.

Kuondolewa kwa maelezo hayo, kuliiondolea Vodacom fursa na haki ya kuwasilisha utetezi wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.


Vodacom haikuridhika na amri hiyo, hivyo ilipaswa kufungua maombi kuiomba mahakama iondoe amri yake lakini ilijikuta imeshachelewa ikalazimika kwanza kuomba kuongezewa muda, yaani kufungua shauri hilo nje ya muda.

Katika shauri hilo la maombi ya madai namba 239/2023, dhidi ya Hadija na Aggrey & Clifford Vodacom ilikuwa ikiomba Mahakama iiongezee muda wa kufungua shauri la maomb, kuiomba Mahakama iondoe amri yake ya kutupilia mbali maelezo yake ya maandishi.

Shauri hilo lilisikilizwa na Jaji Said Ding’ohi kwa njia ya maandishi baina ya Hadija na Vodacom bila kuwapo mdaiwa kwanza, Aggrey & Clifford kwani hakufika mahakamani.


Katika utetezi, wakili wa Vodacom, Gaspar Nyika alidai ilichelewa kufungua shauri kutokana na sababu mbili, kwanza wakati amri inatolewa Machi 9, 2023 haikuwa na taarifa, lakini ilipata taarifa hizo Machi 30, na siku hiyohiyo alienda kudurusu jalada la kesi ya msingi.

Pili, alidai shauri la awali la kuomba kuondolewa kwa amri hiyo lilitupiliwa mbali kutokana na kutokuambatanisha amri ya mahakama iliyokuwa inalalamikiwa.

Alidai kwa kuangalia mazingira ya kesi hiyo na juhudi ilizozichukua kufuatilia kesi ya msingi, kwa masilahi ya haki maombi yake yanapaswa yakubaliwe ili kujipatia haki ya kusikilizwa.

Wakili wa Hadija, Dismas Mallya akiirejesha Mahakama katika uamuzi wa kesi mbalimbali, alidai katika shauri la maombi ya kuongezewa muda, sababu nzuri ya uchelewaji ni ya msingi.

Alidai wakili wa kampuni hiyo hakutoa sababu za kutosheleza, kwani alishindwa kueleza sababu za kuchelewa kwa kila siku aliyochelewa, kuanzia Machi 30, 2023 alipobaini kuwapo kwa amri hiyo mpaka siku alipofungua shauri, na hakuwa mwangalifu kufuatilia shauri la msingi.

Jaji Ding'ohi katika uamuzi ametupilia mbali shauri hilo baada kukubaliana na hoja za wakili Mallya kuwa kampuni hiyo ilichelewa kufungua shauri kuomba kuondolewa kwa amri iliyoondoa maelezo kutokana na uzembe wake.

"Hivyo sababu ya kwanza ya mwombaji (Vodacom) haina msingi", amesema Jaji Ding'ohi baada ya kujadili sababu hiyo na hoja za pande zote.

Amesisitiza mwombaji ameshindwa kueleza siku 21 alizochelewa kutoka Machi 9 mpaka 30, 2023, aliyodai kuwa ndipo alipata taarifa kuhusu kuwapo amri hiyo na siku 10 alizochelewa kutoka Machi 30 mpaka Aprili 11, 2023 alipofungua shauri la kuomba kuondolewa amri ya mahakama na likakataliwa.

Katika hali hiyo aliamua kufuta shauri hilo.

Kesi ya msingi imepangwa kuendelea Alhamisi, Februari 22, 2024 mbele ya Jaji Awamu Mbagwa.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Hadija anadai aliingia mkataba na Vodacom kupitia wakala Aggrey & Clifford Limited Juni 12, 2017, kwa ajili ya tangazo la kibiashara la Vodacom la Red Relax, akiwa mhusika.

Anadai makubaliano yalikuwa tangazo hilo ni kwa ajili ya runinga pekee na si katika mitandao mingine ya kijamii kama vile Youtube, Facebook na mingineyo, na kwa kipindi cha siku 30 kuanzia Juni 12 mpaka Julai 11, 2017, kwa malipo ya Sh500,000.

Licha ya kudai mkataba aupitie kabla ya kusaini, anadai mwakilishi wa Aggrey & Clifford hakumpa mkataba huo bali alimhakikishia tu kuwa ulikuwa umezingatia masharti walivyokuwa wamekubaliana, na hata baada ya kusaini aliomba nakala lakini hakupewa.

Anadai Agosti 2018, alibaini kuwa tangazo hilo lilikuwa limesambazwa kwenye mitandao ya kijamii ya Vodacom, yaani Youtube na Facebook, kuanzia Julai 23, 2017 na limeendelea kuwepo mpaka wakati anafungua kesi hiyo Julai 13, 2022.

Alidai mkataba wake kwa Aggrey & Clifford mpaka akapewa, ndipo akabaini masharti yaliyowekwa katika mkataba yalikuwa ni tofauti na yale walivyokuwa wamekubaliana wakati wa majadiliano.

Mkataba huo anadai uliipa Vodacom haki ya kulitangaza au kuliweka kwenye mitandao yake ya kijamii kadri itakavyoona inafaa kwa muda wa mwaka mmoja na si siku 30 kama walivyokuwa wamekubaliana.

Hivyo anadai yaliyofanywa na Vodacom na wakala yanaonyesha nia ovu ya unyonyaji na kutaka kumpora haki yake au kutumia isivyo halali ujuzi, kazi zake za kisanii na kipaji chake na kumsababishia hasara.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad