Dar es Salaam. Mahakama Kuu imetengua uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kumstaafisha kwa masilahi ya umma aliyekuwa Ofisa Sheria wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Komanya Kitwala.
Kutokana na uamuzi huo Mahakama imemuelekeza Katibu Mkuu Utumishi kufikiria tena maombi ya Kitwala kumrejeshea katika nafasi yake (ajira yake PSSSF) kwa kuzingatia sheria.
Uamuzi huo umetolewa jana Alhamisi, Februari 8, 2024 na Jaji Elizabeth Mkwizu kutokana na shauri la mapitio ya Mahakama, alilofungua Kitwala katika Mahakama Kuu Masjala Kuu Dar es Salaam, akipinga uamuzi wa Rais kumstaafisha utumishi wa umma.
Kitwala akiwakilishwa na Wakili Jeremiah Mtobesya, alifungua shauri hilo dhidi ya Katibu Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bodi ya Wadhamini PSSSF, baada ya kuomba na kuruhusiwa na Mahakama.
Rais Samia alimstaafisha Kitwala, aliyemwandikia barua Katibu Mkuu Utumishi arejeshwe katika ajira yake, baada ya kutenguliwa uteuzi wake wa ukuu wa wilaya.
Mahakama imekubaliana na wakili Mtobesya ikisema uamuzi wa Rais si sahihi kwa kuwa, hauelezi sababu kwa nini alistaafishwa kwa masilahi ya umma.
Jaji Mkwizu amesema suala la masilahi ya umma ni pana, hivyo mtu hawezi kustaafishwa utumishi wa umma kwa maelezo tu kuwa ni kwa masilahi ya umma, bali sababu hizo zinapaswa kubainishwa wazi.
“Kwa hiyo, kwa kutokuelezwa sababu za uamuzi huo kunakiuka matakwa ya maamuzi ya kiutawala,” amesema Jaji Mkwizu baada ya kurejea kesi mbalimbali zilizoamuriwa na Mahakama ya Tanzania kwenye masuala yanayofanana na uamuzi uliokuwa unapingwa na Kitwala.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kitwala amesema hana cha zaidi cha kuongea kwa kuwa huo ni uamuzi wa Mahakama ambao baada ya kusikiliza hoja zake, imejiridhisha kuwa kuna sababu za msingi na ndiyo maana imefikia uamuzi huo.
“Kwa hiyo, Mahakama imeamua kwa kadri ya maombi yaliyopelekwa mahakamani na arguments (hoja) zilizokuwa raised (zilizoibuliwa) mahakamani na mawakili,” amesema Kitwala.
Wakili wa Serikali, Edwin Webiro aliyekuwapo mahakamani kwa upande wa wadaiwa, wakati uamuzi huo uliposomwa hakuzungumza lolote kuhusu uamuzi huo, akiomba apate muda wa kuangalia amri zilizotolewa na Mahakama.
Chanzo cha kesi
Kitwala aliyekuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kuhakiki Mali za Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyoundwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati Dk John Magufuli, aliteuliwa Julai 27, 2018 kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora.
Kwa mujibu wa kiapo kilichounga mkono hati yake ya maombi katika shauri hilo, kabla ya uteuzi alikuwa akifanya kazi PSSSF, akiwa Ofisa Sheria.
Juni 19, 2021 Rais Samia alitengua uteuzi wake na nafasi ilijazwa na Dk Yahya Nawanda.
Kutokana na hilo, Kitwala alimwandikia barua Katibu Mkuu Utumishi, akiomba amrejeshe katika ajira yake ya awali.
Barua hiyo haikujibiwa mapema, lakini baadaye alipokea barua ya Katibu Mkuu Kiongozi ya Agosti 15, 2022, iliyomfahamisha kuwa Rais amemstaafisha kwa masilahi ya umma.
Hakukubaliana na uamuzi wa Rais, hivyo alifungua maombi dhidi ya Katibu Mkuu Utumishi, AG na Bodi ya Wadhamini PSSSF, akiomba kibali cha kufungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama ili kupinga uamuzi wa Rais.
Wajibu maombi waliwasilisha pingamizi la awali, wakiiomba Mahakama itupilie mbali maombi yake bila kuyasikiliza kwa madai yalikuwa na kasoro za kisheria, huku wakiwasilisha hoja mbili.
Mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo na katika uamuzi uliotolewa na Jaji Lilian Mongella Mei 23, 2023 aliridhia maombi ya Kitwala na kumruhusu kufungua shauri kupinga uamuzi wa Rais.
Katika shauri la mapitio, Kitwala aliiomba Mahakama iitishe, kutengua na kutupilia mbali uamuzi wa Rais akidai amekwenda nje ya mamlaka yake kisheria dhidi ya kanuni ya haki asili na ni usumbufu kwake.
Pia, aliiomba Mahakama imuamuru Katibu Mkuu, Utumishi amrejeshe katika ajira yake ya awali kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, kulipwa madeni ya mishahara na mafao mengine kuanzia Juni 28, 2021 mpaka tarehe ya kurejeshwa katika ajira.
Vilevile aliiomba Mahakama iiamuru Bodi ya Wadhamini wa PSSSF kumrejesha katika nafasi yake ya awali.