Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amewataka wananchi wenye kipato cha chini, kutokimbilia mahakamani wanapokuwa na malalamiko yao na badala yake, wawatumie watendaji wa serikali.
Akizungumza na wananchi wa Njombe katika mwendelezo wa ziara zake, Makonda amesema kwa uzoefu wake, anaelewa kwamba mtu akipeleka kesi yake mahakamani, lazima awe na fedha za kumtafuta na kumlipa wakili bora ambaye hataweza kununuliwa na upande wa pili na kupindisha haki.
Amesema hata yeye aliwahi kudhulumiwa nyumba, akashauriwa aende mahakamani lakini kwa kuwa alikuwa anajua kwamba aliyemdhulumu ni mtu mwenye uwezo, hakwenda mahakamani kama alivyoshauriwa.