Mama Mzazi wa Ole Sabaya Afunguka Aliyopitia Mwanae Akiwa Jela



Arusha. Vida Sabaya, mama mzazi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema amepitia kipindi kigumu wakati mtoto wake yuko gerezani.

Vida amesema hayo leo Jumapili Februari 4, 2024 katika ibada ya shukrani iliyofanyika kwenye Kanisa la Ebenezer Restoration Ministry for All Nations, lililopo Moshono, Arusha.

"Sina maneno mazuri, itoshe kusema haya yote ni Mungu amefanya, narudia kusema haya yote ni Mungu amefanya. Ni kweli watu tunapita kwenye mapito mengi, nilichojifunza kwa umri nilio nao wa miaka 63, sijawahi kupita kwenye pito gumu kama hili," amesema na kuongeza:

"Nilibaki nikamwambia Mungu kwa nini mimi, kila mwanamke mwenzangu au wana wa kaya wenzangu au mume wangu ananiambia, ‘mama unapita katika hili kwa sababu Mungu aliona unaweza’."

Amesema: "Na itoshe kusema na niwe mkweli, wako baadhi ya marafiki wanawake wenzangu waliniambia ningekuwa wewe ningekunywa sumu nife au ningeanguka, ila nilisema Mungu ninavyosugua hili goti, iko siku atafanya, sifa na utukufu tumrudishie Mungu, si mwanadamu amefanya."

Kauli ya askofu

Askofu wa Kanisa la Kilutheri Afrika Mashariki (KKAM), Dk Philemon Mollel amesema hawapo kanisani hapo kwa lengo la kumsafisha Sabaya.

"Tumefika hapa kwa ajili ya neno moja tu kumshukuru Mungu kwa matendo makuu aliyofanya kwa ndugu yetu, hatuko hapa kwa sababu ya kumsafisha Sabaya kwenu, lakini tumefika kumshukuru Mungu ambaye tunaamini akisafisha yeye atakuwa safi mbele yake na mbele ya watu wote," amesema.

Amesema, "Sabaya atakuja kujieleza mwenyewe, sisi tunasema gerezani ni mahali pa mateso lakini Wazungu wanasema ni rehabilitation center (kituo cha marekebisho). Kuna watu wamemuona Mungu wakiwa gerezani, Sabaya…shikamana na Yesu maana ndiye atakuinua tena."


Miongoni mwa walioshiriki ibada hiyo ni mawakili waliokuwa wanamtetea Sabaya, Fridolin Bwemelo, Fauzia Mustafa na Emmanuel Ngaiza.

Wengine ni walioshtakiwa pamoja na Sabaya, ambao ni Sylvester Nyegu, Enock Mnkeni na John Odemba.

Pia alihudhuria aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Mary Mnywawi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad