Mashushu wa Simba Waliokwenda Kutazama Mechi za AFCON Wawasilisha Majina ya Majembe Mezani |
Mashushu wa Simba Waliokwenda Kutazama Mechi za AFCON Wawasilisha Majina ya Majembe Mezani
Simba ina mikakati mizito ya kutengeneza kikosi cha ushindani mkali kwa ajili ya msimu ujao (2024/25), tayari imeunda timu ya maskauti iliyosambazwa nchi tofauti kwenda kuangalia wachezaji wenye viwango vikubwa.
Mwanaspoti limepata taarifa timu ya maskauti itafanya kazi kwa awamu mbili, majina yanayopendekezwa kwa sasa yatachambuliwa Machi na mengine Juni, kisha wataamua nani wamsajili.
Kiongozi huyo alisema timu iliyotumwa kuangalia wachezaji kwenye Afcon, Ivory Coast, imepeleka majina mawili mezani. Wanachezea Mauritania. Nahodha anayecheza kiungo namba nane Bodda Mouhsine na beki wa kati Lamine Ba.
Kiungo Mouhsine anaichezea FC Nouadhibou ya nchi kwao na beki Ba anaitumikia NK Varazdin ya Croatia.
“Tulikaa chini na kutafakari ni namna gani tunaweza tukaijenga timu itakayokuwa inanyakua mataji ya ndani na nje, tukaja na mpango mkakati huo, tuliouona utatusaidia na siyo kusajili wachezaji kwa presha, mwishowe wanakuwa hawana msaada.
Pia tutahitaji kuwa na mastaa ambao watakuwa na levo sawa ya viwango na siyo baadhi vinakuwa juu, wanapopata shida timu inakuwa inayumba.”
Hata hivyo, wanachokifanya Simba ni moja ya utaratibu wa kawaida kwa timu nyingi zilizoendelea kwani Sevilla wakati inamwajiri Ramon Rodriguez Verdejo ‘Monchi’ kama mkurugenzi wao wa michezo mwaka 2000, alianzisha kitengo cha maskauti waliopatikana nchi mbalimbali duniani.
Maskauti hao walikuwa 700 na walivumbua vipaji vya mastaa waliosumbua Ulaya kama Diego Capel, Alberto Moreno, Jesus Navas, Antonio Puerta, Sergio Ramos na Jose Antonio Reyes.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Steven Mapunda alisema; “Kama Simba imeanza na utaratibu huo, utaleta mapinduzi makubwa na inaweza ikachukua ubingwa hadi wa CAF kwani itakuwa ina uhakika na ubora wa wachezaji wanaowasajili.”
Beki wa zamani wa timu hiyo, Amir Maftah alisema “Kinachofanywa na Simba ni kawaida kwa nchi zilizoendelea, hivyo zoezi hilo likifanikiwa litaizalia matunda ya ushindani wa Ligi ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.”