YANGA V/s CR BELOUIZDAD ni mchezo mgumu kwa sababu kila timu inahitaji kupata alama tatu ili kuweka hai matumaini ya kufuzu hatua ya Robo Fainali.
Kwenye kundi hili Al Ahly tayari imefuzu hatua ya Robo Fanali baada ya jana kushinda ugenini dhidi ya Medeama, Yanga na Belouizdad zinaweza kufikisha alama tisa ambazo Al Ahly inazo lakini Medeama haiwezi kufikisha alama hizo.
Kwenye hesabu za karatasi Medeama bado ina nafasi ya kufuzu Robo Fainali, ikiwa Yanga na Belouizdad zitatoka sare leo zitakuwa na alama sita, Yanga ikipoteza mchezo wa mwisho dhidi ya Al Ahly halafu Medeama ikashinda mechi ya mwisho dhidi ya Belouizdad itafikisha alama saba na kwenda hatua inayofata.
Yanga leo ikichukua alama tatu mbele ya Belouizdad itafikisha alama nane, alama moja nyuma ya Al Ahly ambayo ina alama tisa na tayari imefuzu kucheza Robo Fainali.
Belouizdad wanafahamu leo ndio fainali yao, watataka kupata walau alama moja ili wasiachwe mbali na wapinzani wao [Yanga] kuwania nafasi ya kuungana na Al Ahly.
Kwa hiyo ni kundi ambalo bado lipo wazi kwa Belouizdad na Yanga hadi mechi za mwisho kujua ni timu gani ambayo itaondoka pamoja na Al Ahly kwenda Robo Fainali.