WAKATI mjadala ukiendelea kushika kasi juu ya shutuma alizozitoa mshambuliaji wa Pyramids Fiston Mayele, limeibuka jipya baada ya meneja wake aliyemleta nchini Nestor Mutuale kutoa neno kuhusu Mkongomani huyo.
Mutuale ameliambia Mwanaspoti kwa simu akiwa DR Congo kuwa endapo madai yanayoenea yatakuwa yametoka kwa Mayele, mshambuliaji huyo atakuwa ameikosea heshima klabu yake hiyo ya zamani ya Yanga.
Mutuale amesema hata kama Mayele atakuwa amekasirishwa na shabiki mmoja wa soka, au kiongozi fulani, hakuwa sahihi kuisema vibaya timu ya Yanga ambayo ina mchango mkubwa kwenye maendeleo yake.
“Nimeona mitandao ya Tanzania inasema hayo mambo kwamba Mayele anaisema vibaya Yanga, sijaongea naye tangu wamerudi hapa nchini kutoka Ivory Coast, lakini kama kweli hayo maneno ameyasema yeye atakuwa ameikosea heshima Yanga,” amesema Mutuale.
“Wachezaji hawatakiwi kuwajibu mashabiki hasa mitandaoni, shabiki anaweza kusema lolote, mchezaji unatakiwa kuvumilia na kuendelea kufanya kazi yako, kule uwanjani ndio unatakiwa kuwajibu mashabiki.
“Yanga haiwezi kufanya kitu kibaya kwa Mayele, kama kuna shabiki amemtolea lugha chafu Mayele atakuwa amekosea lakini Mayele kuisema vibaya Yanga ni makosa makubwa amefanya.
“Unajua Yanga imefanya makubwa kwa Mayele, ule upendo walimpa ni wa kiwango kikubwa sana, wapo watoto, wakubwa, viongozi na maelfu ya mashabiki wamekuwa wakimpenda Mayele kutokana na kazi yake, unapotaka kusema kitu kibaya kuhusu mtu mmoja unatakiwa kuwaangalia hawa wengi watajisikiaje.
Aidha, Mutuale amewataka mashabiki wa Yanga kumsamehe Mayele kwani atakuwa amejifunza kuwa amekosea kwani bado ni mtoto wao ambaye siku moja wanaweza kukutana naye tena.
“Mimi nitamtafuta Mayele nitaongea naye, nimeongea na viongozi wa Yanga wamesikitika, lakini nimewaambia wamsamehe Mayele na mashabiki nao wamsamehe ni mtoto wao amewakosea hawawezi kusema sio ndugu yao tena, maisha yanaweza siku moja tena yakamfanya arudi tena nyumbani kwao Yanga.”
Mitandao ya kijamii imelipuka kwa watu kufanyiana utani kwamba wanayanga wanamfanyia hujuma Mayele asifunge mabao katika klabu yake ya Pyramids na timu yake ya taifa ya DR Congo.