Milima, Mabonde Safari ya Lowassa Kuusaka Urais Tangu Mwaka 1995

Milima, Mabonde Safari ya Lowassa Kuusaka Urais Tangu Mwaka 1995


Waziri Mkuu aliyejiuzulu wadhifa huo, Edward Ngoyai Lowassa amefariki dunia jana Jumamosi, Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango, wakati akitangaza kifo chake amesema Lowassa (70) amefariki dunia akiendelea na matibabu ya magonjwa ya kujikunja utumbo, matatizo ya mapafu na shinikizo la damu.


Hii inamaanisha hatutamuona tena katika ulimwengu huu, lakini Watanzania watakumbuka nguvu ya kisiasa aliyokuwa nayo na safari yake ya kuusaka Urais ilivyoanza mwaka 1995.


Waziri mkuu mstaafu na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema 2015, Edward Lowassa aliripoti katika makao makuu ya Polisi kwa kosa la kutoa kauli ya uchochezi kuhusiana na Waisilamu wa kundi la Uhamsho waliopo mahabusu.


Uchaguzi siku zote huja na mvumo wake, lakini uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995 na ule wa 2005 ndio ulikuwa na mvumo mkubwa kutokana na kuibuka kundi la ‘Boys 2 Men’ lakini leo mmoja wa Boys 2 Men Hatunaye.


Kwa wasiofahamu, kundi la ‘Boyz 2 Men’ liliwahusu marafiki wawili wakubwa wa wakati ule, Jakaya Kikwete na Edward Lowassa lakini leo Lowassa hatunaye baada ya kufariki dunia akipatiwa matibabu JKCI.


Ni nguvu za wawili hao baada ya kukosa nafasi ya kuteuliwa kugombea urais uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ndipo 2005 wakakubaliana Kikwete ndiye agombee na Lowassa amuunge mkono.


Maandiko mengi ambayo hayajakanushwa kikamilifu, yanasema wawili hao walikubaliana JK aanze mihula miwili (2005-2015), halafu amsapoti Lowassa kuwa Rais kwa muhula unaofuata yaani uchaguzi wa 2015 na ule wa mwaka 2025.


Waziri wa zamani, Edward Lowasa akionyesha fomu ya kuwania nafasi ya uras 2015 kwa tiketi ya Chadema.


Haikuwa rahisi kupenya mwaka 1995 kutokana na kizingiti cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye tangu walipochukua fomu za urais wakasafiri pamoja kwa ndege, kwani inaelezwa hakuupenda urafiki wa wawili hao.


Lowassa inaelezwa ndio aliutaka sana urais mwaka ule lakini aliamua kujificha nyuma ya Kikwete kwa sababu Nyerere alikuwa ameshatilia shaka uadilifu wake, kutokana na utajiri aliokuwa nao licha ya kwamba si dhambi kuwa tajiri.


CCM ikarejesha majina matatu tu ambayo yalipelekwa kwenye ngazi ya juu ya mchujo, jina la Lowassa halikuwapo kwani tayari baba wa Taifa ambaye aliheshimika sana, inaelezwa alikuwa ametilia mashaka utajiri wake.


Katika mzunguko wa kwanza wa kura za maoni, Kikwete aliibuka mshindi kwa kupata kura 534, akifuatiwa Benjamin Mkapa ambaye baadaye alikuja kuwa Rais kwa kupata kura 459 na mzee Cleopa Msuya aliyepata kura 336.


Hata hivyo, upigaji kura ulienda mzunguko wa pili kwa maelezo kuwa Kikwete hakupata kura nyingi (simple majority) kati ya kura 1,331 zilizopigwa na wajumbe wa CCM, hivyo mzunguko wa pili, Mkapa akapata 686 na Kikwete 639.


Kwa mujibu wa utafiti wa British Academy, matokeo hayo yalikuwa na utata na yalipingwa na kulikuwa na hisia kuwa Nyerere ndio aliingilia kati na kuhakikisha Mkapa ndio anasimama kugombea urais.


Kulingana na matokeo hayo ilikuwa ni dhahiri kuwa Nyerere hakuwa anajua vizuri nguvu ya ‘Boyz 2 Men’ kwa sababu kama angeijua, asingeruhusu Kikwete afike mbali kiasi hicho kwenye kura na wawili hao hawakuacha matamanio yao ya urais. Lowasa kujiunga Chadema


Nyerere anachukuliwa kama mwadilifu na aliyetumika kuvunja makundi yasiyo rasmi kuchukua madaraka mwaka 1995, alifariki dunia 1998 hapo ndipo zilipozaliwa siasa mpya ndani ya CCM kwa kuzaliwa mitandao minne.


Kwa mujibu wa utafiti huo uliofadhiliwa na British Academy na DFID za Uingereza, kifo cha Nyerere kilishuhudiwa ikizaliwa mitandao minne ikitafuta urais 2005 baada ya Mkapa na moja ni kundi la Boys 2 Men la Lowassa na Kikwete.


Inaelezwa katika utafiti huo kuwa kundi hili liliendelea kujipenyeza ndani ya mifumo ya CCM lilifanikiwa kuwaingiza katika mtandao huo, Dk Emmanuel Nchimbi wa UVCCM na Sophia Simba wa Umoja wa Wanawake wa CCM.


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisalimian na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho Edward Lowassa wakati wa moja ya mikutano ya ndani ya chama hicho 2015 kuelekea uchaguzi mkuu.


Mtandao wa pili ulikuwa ni wa Profesa Mark Mwandosya uliotaka urais uwe zamu ya kusini, kundi la tatu la Waziri mkuu, Frederick Sumaye na kundi la nne lilikuwa ni la Waziri mkuu mstaafu na mwenyekiti mstaafu wa OAU Salim Ahmed Salim.


Uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ulipowadia, Lowassa na Kikwete kila mmoja akawa anautamani urais, kiasi kwamba kama sio Mzee Peter Kisumo kuingilia kati na kukutana nao na kutaka wakubaliane kuachiana, pengine wangegawana kura.


Kundi hili la ‘Boyz 2 Men’ na mtandao wake likafanya kazi kubwa hadi Kikwete akaibuka kidedea kwa kupata kura za kishindo katika mchujo ndani ya CCM mwaka 2005 zikiwa 1,072, Salim kura 476 na Profesa Mwandosya akapata kura 122. Hatima ya Lowasa Chadema


Boys 2 Men likatoa spika, waziri mkuu


Mbali na Kikwete na Lowassa, lakini mtandao huo uliwajumuisha vigogo kama, Rostam Aziz na Nazir Karamagi waliokuwa wafanyabiashara mashuhuri, Samwel Sitta, Dk John Nchimbi, Sophia Simba na Kisumo waliokuwa na nguvu kubwa kisiasa.


Ni kundi hilo ndilo inaelezwa lililopanga Sitta awe Spika wa Bunge la tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Lowassa awe waziri mkuu na hata wakati Sitta anasoma bungeni jina la waziri mkuu ili lipigiwe kura, halikuwa geni.


Ni katika kipindi cha utawala wa Kikwete ndipo kundi la wanamtandao lilipoanza kuparanganyika na kukiletea CCM wakati mgumu katika uchaguzi mkuu wa 2010 na ule wa 2015, ambapo Lowassa na Kikwete wakaanza kuhitilafiana.


Bunge chini ya Sitta likamsulubu Lowassa kutokana na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe, kuhusu kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, hadi Lowassa akaamua kujiuzulu uwaziri mkuu, Februari 7, 2008.


Lowassa na uchaguzi mkuu 2015


Hadi kuelekea uchaguzi mkuu 2015, inaelezwa ndani ya CCM, Kikwete alikuwa amesimama upande wa Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati ule, Benard Membe, huku Lowassa akibebwa na mitandao mingine ukiwemo Friends of Lowassa.


Wanamtandao wawili waliobebana 1995 na 2005 ndio sasa walikuwa wakichuana na kupingana na mwisho wa siku, Lowassa ndiye aliyepoteza vita hiyo.


Aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati Dk John Pombe Magufuli akiagana na Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Hayati Edward Lowassa baada ya kuutangazia umma rasmi kwamba anarudi nyumbani. Kushoto ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walipokutana katika Ofisi Ndogo za Makao makuu ya CCM mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam Ijumaa March 1, 2019. PICHA NA IKULU


Lowassa jina lake lilikatwa mapema hata hakufika kwenye tano bora, lakini kwa vile aliutaka urais kufa na kupona, alijiunga na Chadema na kufanikiwa kuteuliwa kupeperusha bendera ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini akaangushwa na Hayati John Magufuli.


Katika kampeni zake, Lowassa hakuacha kuficha hisia zake pale aliposema majukwaani kuwa alitarajia Kikwete angemuunga mkono ndani ya chama 2015, lakini alimgeuka, na ni mvurugano wao ndio iliomuibua Magufuli na kuwa Rais.


Lowassa alinukuliwa akisema alitarajia Kikwete angemsaidia kwa vile walikuwa na makubaliano kwamba yeye amsaidie 2005 ili aweze kushinda na ndio maana wala hakumpinga 2010, akiamini uchaguzi wa 2015 naye angemuunga mkono. Baada ya kuangushwa na Magufuli na Ukawa iliyokuwa na vyama vinne CUF, NCCR-Mageuzi, NLD na Chadema kugomea kutambua matokeo hayo na kukawa na vuguvugu la kuitisha maandamano makubwa nchini, Ni Lowassa ndiye aliyetuliza joto hilo na aliponukuliwa akisema hautaki urais wa damu.


Rais Jakaya Kikwete akimnadi mgombea Ubunge jimbo la Monduli, Edward Lowassa wakati wa uchaguzi wa Mwaka 2010.


Akiwajibu wale waliotaka yeye, Chadema na Ukawa waingie barabarani, Lowassa alisema kama angefanya hivyo, wangekuwa wanakwenda Ikulu kwa kumwaga damu za Watanzania wasio na hatia ambao wangepata madhara.


“Tutakuwa tunakwenda Ikulu kwa kufagia barabarani kwa damu za watu. No (hapana), Tutakwenda Ikulu bila damu za watu wakati wowote na Mungu atatusaidia. Nawaambia wale wote ambao hawakuridhika, mnajua nguvu ya umma lakini msiitumie kuwaumiza watu,” alinukuliwa Lowassa akisema.


Baadaye Machi 1, 2019, Lowassa akatangaza kurejea tena CCM na hadi umauti unamkuta alikuwa mwanachama safi wa chama hicho tawala. Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina Lake Lihimidiwe. Pumzika kwa amani Lowassa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad