Mjane wa 'nyama ya swala' asema hakimu aliyemhukumu asilaumiwe

 


Jana katika sehemu ya kwanza ya mazungumzo haya, Maria Ngoda alieleza namna faraja kutoka kwa wafungwa wenzake na askari wa Jeshi la Magereza zilivyomfanya abadili kusudio lake la kujiua akiwa gerezani baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 22 gerezani.


Novemba 3, mwaka jana, mjane huyo alihukumiwa kifungo hicho baada ya kukutwa na hatia ya kukamatwa akiwa na vipande 12 vya nyama ya swala, hukumu iliyozua mjadala mkali kitaifa, hata kukatiwa rufani.


Maria, katika mazungumzo na Nipashe, amesema wapo watu wanamlaumu hakimu aliyetoa hukumu, lakini yeye haoni kosa kwa hakimu huyo.


Amesema makosa yako kwake (Maria) kwa kukiri kutenda kosa kutokana na kile alichodai kuelekezwa kufanya hivyo na waliomkamata; walimtaka akubali yaishe, hakimu akatoa hukumu kutokana na mshtakiwa kukiri kutenda kosa.


"Ukweli niliutoa mimi mahakamani, hivyo hakimu asilaumiwe, zaidi ya kumwombea kwa Mungu mambo yake yazidi kunyoka kwani hana kosa lolote," amesema Maria.


Akizungumzia mazingira ya kukamatwa kwake Maria amedai kuwa wakati anakamatwa, alikuwa jirani na ndoo ambayo aliachiwa na mtu anayeitwa Fute ili "amtazamie" na hakujua ndani mna nini, ghafla walitokea watu ambao ni askari pamoja na mwenyekiti wa mtaa ambao walikuwa wakimvizia Fute, lakini mtuhumiwa huyo wa uhalifu aliwashtukia na kukwepa mtego huo, akitelekeza mzigo huo kwa mjane huyo.


"Walipofika eneo la tukio waliuliza 'mwenye ndoo hii ni nani?' Niliwaambia '...ni Fute katoka kidogo'. Wakaniomba nifunue mfuniko wa ndoo, baada ya kufunua..., eneo la tukio walibaki watu wengine, mimi na wao tuliondoka kwenda kwa Fute japo nyumbani hatukumkuta ila mazingira ya kwake tulikuta yakiwa na vielelezo vya nyama pori.


"Baada ya kutoka hapo, tulikwenda nyumbani kwa mwanamke mmoja ambako tulikuta nyama nyeusi ikiwa imechomwa kwa ajili ya kuuza waliichukua na kupakia kwenye gari bila mhusika huku wakijisemesha 'Maria atakwenda kuisaidia Jamhuri' kisha walifika eneo la ndoo na kuniambia nipakie ndoo kwenye gari na kwenda polisi huku wakinitaka kukiri kosa kuwa nyama ile ya swala ni yangu. Kwa kweli niliumia sana."


Maria amewashukuru Mawakili wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambao walimsaidia kutoka gerezani, akitoa shukrani mahususi kwa Mwanaharakati Vitus Nkuna ambaye alisambaza taarifa ya hukumu yake iliyopelekea makundi mbalimbali kuonesha kuguswa na kuanza kumsaidia wakiwamo UWT pamoja na waandishi wa habari kwa umoja wao, akisisitiza kuwa alipata faraja kubwa.


"Huyu Nkuna simjui tu ila nilitamani kukutana naye hata nikambeba mgongoni maana sina zawadi nyingine ya kumpa ila nikiwa gerezani alikuja MNEC Salim Abri (Asas) na kuniulizia 'yule mama aliyefungwa miaka 22 yuko wapi? Niliishia kumtazama lakini nilitamani kumpa mkono ila taratibu za Magereza hazikuruhusu mimi kumpa mkono wa pongezi, hivyo ninatafuta siku nikutane naye ili kumshukuru na kumwomba yeye na Rais Samia Suluhu Hassan wanisaidie kunijengea nyumba ya kuishi maana sina nyumba ya kuishi," amesema Maria.


Pia amesema kuwa kwa sasa anatamani kufanyabiashara ndogo itakayomwingizia kipato kwa kuwa biashara yake ya awali ilikuwa kuponda kokoto au kuuza mboga za majani mitaani, lakini sasa anatamani kufungua kioski cha bidhaa mbalimbali.


Maria pia amewashukuru wadau mbalimbali ambao wameendelea kumsaidia na kuahidi kumsaidia mtaji ikiwamo Taasisi ya Sauti ya Haki Tanzania pamoja na Kampuni ya Uwakili ya BLS ambao walijitokeza kumsaidia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad