Mudathir Anavyovunja Rekodi zake Mwenyewe

 

Mudathir Anavyovunja Rekodi zake Mwenyewe

“Leo nikipata tena nafasi nitafunga tena, hapa ni nyumbani kwangu hakuna nisichokijua katika uwanja huu.” Haya ni maneno ya Mudathir Yahya kabla ya mchezo dhidi ya Mashujaa katika Uga wa Chamazi.


Mkeka wa Privaldinho


Mudathir amekuwa na mwendelezo mzuri sana hivi karibuni kwa kufunga magoli muhimu licha ya kwamba jukumu lake asilia ni kiungo wa kati. Pengine tulidhania kwa kuwa anaifahamu vizuri Chamazi basi atatamba Chamazi pekee, lakini ameendeleza moto ule ule mpaka mpaka uwanja wa Jamhuri. Kwa ufupi, Mudathir hana shughuli ndogo, popote anakamua.


Kufikia sasa Mudathir Yahya amefunga takribani magoli 6, ukiwa msimu wake bora kabisa, ukiachana na msimu wa 2020/21 ambao Mudathir alifunga magoli matatu na kutoa pasi sita za mabao.


Mudathir alijitambulisha rasmi kwenye soka la Tanzania miaka 8 iliyopita alipokuja Dar es Salaam kushiriki michuano ya Copa Coca Cola na timu yake ya Mjini Magharibi, makocha wengi na wadau walikoshwa sana uwezo wake wa kumiliki mipira na upigaji wake wa mashuti na pasi za uhakika.


Mudathir alifanya mazoezi katika uwanja wa Tamco ambapo alikutana na swahiba wake Farid Mussa Maliki ambaye nae alikuwa akitokea mkoani Kilimanjaro kwa wakati huo.


Pengine vijana hawa wakati wakiwa kwenye safari yao ya matumaini hawakujua kama ipo siku watavaa medali ya CAF wakiwa na klabu namba mbili kwa ushawishi barani AFRIKA.


Mudathir amekuwa mhimili mkubwa sana kwa Yanga SC tokea amejiunga nasi. Muunganiko wake na Khalid Aucho pamoja na magwiji wengine umekuwa nguzo na chachu ya mafanikio ya Yanga SC.


Sifa kubwa ya Mudathir kunusa hatari aidha kwa upande wa klabu yake ama kwa wapinzani, anakaba na kuondoa mipira ya hatari kwa nidhamu ya hali ya juu. Sio mbabaikaji pale ambapo anahitajika kufanya maamuzi sahihi kwa maslahi ya usalama wa timu.


Ukiachana na sifa yake kuu ya kuingia uvunguni na kuchukua mali, amezidi kutonesha kuwa Magoli yake mawili jana dhidi ya KMC FC ametuonesha kuwa miongoni mwa wachezaji hatari sana msimu huu kwani amefunga magoli muhimu na dakika za kisu shingoni.


Wakati zikiwa zimesalia dakika ambazo zinamruhusu njiwa kumeza punje ya mtama pekee, Mudathir yeye anaamini kuwa dakika hizo zinamtosha kumlisha hata sisimizi tikitimaji na akamaliza.


Ni mpambanaji ambaye hakati tamaa, ambaye anaheshimu kila sekunde na kila dakika, hakati tamaa na anajua kuwa atafutaye ndiye apataye, Mudathir mechi ya Dodoma Jiji alifunga bao la ushindi dakika 85, mechi na Mashujaa amefunga bao la ushindi dakika ya 85.


Wakati mashabiki wakiwa jukwaani na presha kuwa tutafunga saa ngapi, Mudathir ana mawazo tofauti kabisa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad