Mungu Aendelea Kumpigania Sabaya, Ambwaga Tena DPP Mahakamani




Arusha. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, amembwaga tena kortini Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ambaye rufaa aliyokata na kuanza kusikilizwa, Mahakama ya Rufani imeamuru mwenendo wake usikilizwe upya.

Hiyo ni baada ya jopo la majaji watatu, Ferdnand Wambali, Patricia Fikirini na Jaji Issa wa Mahakama ya Rufani walioketi jijini Arusha kutoa hukumu juzi ya kufuta mwenendo, uamuzi na amri ya Mahakama ya kuanzia Desemba 12 hadi 14, 2022.

Awali, Sabaya na wenzake Enock Mnkeni, John Odemba na Sylvester Nyegu walifungua maombi mahakamani hapo dhidi ya DPP, wakidai Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu Arusha, kakiuka taratibu za uendeshaji wa rufaa ya DPP.

DPP alikata rufaa dhidi ya Sabaya na wenzake, akipinga kuachiwa kwao katika kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa ikiwakabili, wakituhumiwa kuchukua rushwa ya Sh90 milioni kutoka kwa mfanyabiashara Francis Mrosso Januari 22, 2021.

Sabaya na wenzake waliachiwa huru Juni 10, 2022 na Hakimu Mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Dk Patricia Kisinda ambaye alisema ushahidi uliotolewa ulikuwa na utata na hati ya mashitaka ni upungufu hivyo kushindwa kuthibitisha mashitaka hayo.

Hata hivyo, DPP hakuridhika na uamuzi huo na kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha na kupangiwa Jaji Maghimbi kuisikiliza lakini katikati ya usikilizwaji wake, Sabaya na wenzake hawakuridhika na mwenendo wa kesi.

Kupitia kwa mawakili wao Moses Mahuna, Fauzia Mustafa, Fridoline Bwemelo na Sylvester Kahunduka, walifungua maombi ya jinai namba 3/2023 wakidai Jaji alisikiliza pingamizi la Sabaya bila uwepo wa warufani wengine watatu.

Hoja nyingine waliyoegemea ni kuwa Jaji hakuwapa nafasi rufani wa pili Enock Mnken, John Odemba (wa tatu) na Sylvester Nyegu (nne)haki ya kusikilizwa katika pingamizi hilo kwa kuwa wakati linasikilizwa, walikuwa hawajapewa wito.


Hii inakuwa ni kesi ya tatu kwa Sabaya na wenzake kumshinda DPP, baada ya Mei 6, 2022 kushinda rufaa ya kupinga kifungo cha miaka 30 walichohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa makosa ya unyang’anyi wa makundi.

Hiyo ni baada ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo kuona upande wa jamhuri ulikuwa umeshindwa kuthibitisha mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha dhidi ya Sabaya na wenzake na kuwatia hatiani unyang’anyi wa makundi.

DPP hakuridhika kuachiwa huru kwa Sabaya na wenzake Mahakama Kuu ya Arusha, akaamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani; na ilipofika Novemba 17, 2023 jopo la majaji watatu liliitupa wakisema Jaji wa Mahakama Kuu alikuwa sahihi.

Hoja za kisheria zilivyokuwa


Akijenga hoja kwa niaba ya Sabaya na wenzake, mbele ya jopo la majaji, wakili Mahuna alisema mwenendo wa shauri la rufaa ya DPP wa Desemba 12 hadi 14, 2022 ulitawaliwa na dosari za kisheria, hivyo kuwaathiri warufani Mnkeni, Odemba na Nyegu.

Akifafanua nini kilichotokea mbele ya Jaji Maghimbi, wakili Mahuna alisema ingawa mrufani namba moja (Sabaya) alikuwepo kortini Desemba 12, 2022 baada ya kupokea wito rasmi, hakuwa amepokea sababu za rufaa.

Mahuna aliieleza Mahakama kuwa siku iliyofuta, Sabaya na mawakili wake na mrufani wa nne (Nyegu), walikuwepo, lakini Nyegu hakuwa na wakili.

Kutokana na hilo, wakili Mahuna aliwasilisha pingamizi la awali (PO) na kuwasilisha hoja juu ya pingamizi hilo.

Kwa mujibu wa wakili Mahuna, baada ya kumaliza kuwasilisha hoja zake, Jaji Maghimbi hakujishughulisha kumpa nafasi Nyegu kuwasilisha hoja zake kuhusu pingamizi hilo la awali lililokuwa limeibuliwa na wakili wa Sabaya.

Badala yake, Jaji Maghimbi akamwalika DPP kujibu, na alifanya hivyo; lakini kumnyima Nyegu nafasi ya kuieleza Mahakama lolote juu ya pingamizi hilo ni kumnyima haki ya kusikilizwa ambayo ni nguzo muhimu ya haki ya asili.

Wakili Mahuna akaendelea kuwaeleza majaji hao watatu kuwa, uamuzi kuhusiana na pingamizi hilo la awali, ulitolewa Desemba 14, 2022 mbele ya Sabaya na mawakili wake na Nyegu, bila uwepo wa Mnkeni na Odemba ambao hawakuwa wamepata wito.

Akijibu, wakili mwandamizi wa Serikali Patrick Mwita akisaidiana na mawakili wa Serikali waandamizi, Abdalah Chavula, Kevin Kihaka, Felix Kwetukia na Timothy Mmari, alipinga hoja za kina Sabaya na mwenzake walizowasilisha kortini.

Wakili huyo alisema katika hoja zao kina Sabaya wameshindwa kueleza ni kwa vipi waliathiriwa na mwenendo, uamuzi mdogo na amri maelekezo ya Mahakama yaliyotolewa na Jaji Maghimbi kati ya Desemba 12, 2022 na Desemba 14, 2022.

Pia, alijenga hoja kuwa maombi hayo yameharakishwa kwa sababu rufaa yenyewe ya DPP haijasikilizwa, siku ilipopangwa kusikilizwa Desemba 13, 2022 Sabaya na Nyegu walikuwepo na pingamizi la awali lilijadiliwa na mawakli wa Sabaya.

Kuhusu hoja ya Nyegu ambaye hakuwa na wakili kutopewa nafasi ya kujadili pingamizi la awali, wakili Mwita, alikiri mrufani huyo kutopewa haki hiyo ya kusikilizwa na Mahakama, lakini akashangaa hilo lilimuathiri vipo mrufani huyo.

Kuhusu Mnkeni na Odemba kutopewa wito wa kuitwa kortini, wakili huyo alisema waombaji hao walipelekewa wito huo kupitia ofisi ya RCO Arusha baada ya kubaini wengine hawapatikani, waliomba kutoa matangazo magazetini.

Wakili Mwita akaeleza jopo hilo la majaji kuwa baada ya kutoa matangazo, Mnkeni na Odemba wangeweza kwenda mbele ya jaji na kumuomba awasikilize badala ya kutumia njia ya kuwasilisha maombi ya jinai kama walivyofanya dhidi ya DPP.

Uamuzi wa jopo la majaji

Baada ya kusikiliza hoja za kisheria za pande zote mbili, jopo la majaji hao watatu waliegemea katika hukumu mbalimbali za Mahakama hiyo, zilizosisitiza haki ya kusikilizwa ni haki ya msingi.

Mbali na msimamo huo wa kisheria, lakini majaji hao walisema Ibara ya 13(6(a) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na marekebisho yake, imesisitiza umuhimu wa mtu kupata haki ya kusikilizwa.

Walinukuu ibara hiyo kuwa, “wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa Mahakama au chombo kingine, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu na haki ya kukata rufaa.”

Majaji hao walisema kwa kutazama mwenendo unaolalamikiwa, hawawezi kumung’unya maneno kwamba waombaji wa pili, watatu na wa nne hawakupewa haki ya kusikilizwa, bali ni dosari haipaswi kuachwa bila kurekebishwa.

“Mwenendo wa shauri hilo wa kuanzia Desemba 12 hadi 14, 2022 na uamuzi wa Mahakama uliofikiwa bila ushiriki kwa muombaji wa pili, wa tatu na wa nne hauwezi kuachwa kama ulivyo kwa kuwa unakiuka haki ya asili,”alisema mmoja wa majaji kwa niaba.

Majaji hao wakasema, kwa mamlaka ya kisheria ambayo Mahakama ya Rufani inayo, mwenendo, uamuzi na amri inayolalamikiwa ya Desemba 12 hadi 14, 2022 inafutwa na jalada lirejeshwe Mahakama Kuu kulisikiliza kuanzia kwenye pingamizi la awali.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad