Msemaji wa Simba Sc Ahmed Ally ametupa jiwe kichakani kwa kudai kuwa mara ya mwisho Simba ilifuzu robo fainali mechi ya mwisho ya hatua ya makundi kwa kumfunga mtu 7-0.
Ahmed amewaambia waandishi wa habari kuwa anawashangaa majirani kwa kuchanganyikiwa na goli nne pekee.
Ahmed amewataka mashabiki wa Simba kujiandaa vyema kuishangilia timu yao siku ya Jumamosi.
“Mechi dhidi ya Jwaneng Galaxy itachezwa Jumamosi Machi 2, 2024 saa 1:00 usiku. Licha ya mapendekezo yetu kucheza mechi saa 10:00 jioni lakini CAF wameamua iwe saa 1:00 usiku ili michezo yote iwe muda mmoja.”
“Kikosi kimerejea nchini na leo jioni tutaanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo Jwaneng Galaxy na mchezo wa ASFC dhidi TRA ambao tutacheza Jumatano kwenye uwanja wa Azam Complex.”
“Waamuzi wa mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy wataanza kuwasili nchini kuanzia tarehe 29 mwezi huu na wote wanatokea nchini Ghana.”
“Mpaka sasa hatujapata taarifa rasmi Jwaneng Galaxy lini watawasili nchini lakini watu wao wa maandalizi ya awali wameshawasili nchini.”
“Ushindi wa aina yoyote ambao tutapata Jumamosi sisi tutafuzu bila kujali Wydad kapata ushindi wa aina gani. Sisi na Wydad tukishinda tutakuwa na alama tisa na kanuni ya kwanza ya CAF inaangalia Head to Head, mechi ya kwanza walitufunga goli 1-0 na sisi tukawafunga 2-0.”
“Tukifanikiwa kufuzu robo fainali tutakuwa tumeungana na timu zingine kubwa barani Afrika ambazo zimewahi kuingia robo fainali mara nne mfululizo. Hapa nazungumzia Al Ahly, Mamelodi, Wydad na TP Mazembe na sisi tunakwenda kuwa timu ya tano.”
“Tangu tumeanza kampeni ya kimataifa hatujawahi kuishia hatua ya makundi, hatujawahi kufungwa mechi ya mwisho ya maamuzi ya kwenda robo fainali. Simba Sports Club inapofika hatua kama hii anakuwa mnyama mwingine wa ajabu.”
“Hatujawahi na hatutakuja kuishia hatua ya makundi, achana na watu wanaochanganyikiwa na ushindi wa goli 4, Mnyama tumeshamfanya mtu goli 7 na tukaenda robo fainali.”- Ahmed Ally.